Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, ameiomba Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwezesha zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Meru baada ya kukamilisha zoezi hilo katika Halmashauri nyingine za mkoa wa Arusha.

Mhe. Kaganda amesema hatua hiyo itasaidia mkoa mzima kuwa na takwimu safi za Anwani za Makazi na hivyo kuwezesha masuala yote muhimu yakiwemo ya upangaji wa mipango ya maendeleo kufanyika kwa ufanisi.

Ametoa wito huo tarehe 30 Agosti, 2024 wakati akizungumza na timu ya Wataalamu wa Anwani za Makazi na Mradi wa Tanzania ya Kidigitali iliyo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari waliofika ofisi kwake pamoja na mambo mengine kumpa mrejesho wa zoezi hilo la uhakiki lilivyofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Arusha.

Mhe. Kaganda ametoa msisitizo huo kwa Mratibu wa Anwani za Makazi Taifa Mhandisi Jampyon Mbugi na Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) Bw. Bakari Mwamgugu kuhakikisha zoezi la uhakiki linafanyika katika Halmashauri ya Meru ikizingatiwa kuwa ni zoezi muhimu kwa Halmashauri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Seleman Msumi ameipokea timu ya waratibu hao ofisini kwake na kupongeza zoezi la uhakiki lilivyoendeshwa katika Halmashauri yake na kwamba wataendelea kuunga mkono kwa kushirikiana na waratibu wa Wilaya.

Mhandisi Mbugi na Bw. Bakari wakizungumza na viongozi hao kwa nyakati tofauti wameeleza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na waratibu wa Wilaya pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Anwani za Makazi na namna zinavyochangia kukuza uchumi hususan uchumi wa kidijitali.

Zoezi la uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi ni zoezi muhimu linalotekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Share To:

Post A Comment: