BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2024 wenye mambo kadhaa yanayolenga kuondoa changamoto zinazowakabili wanachama na utaratibu wa upatikanaji wa mafao.


Marekebisho hayo yanagusa Sheria tatu ambazo ni Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50, Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Sura ya 371, na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263.

Akiwasilisha maelezo ya muswada huo bungeni Agosti 29, 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema marekebisho hayo yanatokana na nia ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutatua changamoto ikiwamo mkwamo wanaoupata watumishi wanapostaafu.

Pia, amesema muswada huo umelenga kutatua suala la wastaafu hao kukutana na kizingiti cha Waajiri kutowasilisha michango kwa wakati kwenda kwenye Mifuko na kuongeza makusanyo.

“Pia unalenga kuondoa changamoto ya uonevu wakati wa kuwapatia haki wafanyakazi wanaoumia makazini na anayepaswa kutoa taarifa anaposhindwa kutoa taarifa ndani ya muda; malipo yasiyo ya lazima na kulinda watumishi katika stahiki zao; kwa Waajiri kuwapa ulinzi wa taarifa, na kuwajengea mazingira wachangie na kuwapa nafuu katika malipo,”amesema.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq amesema kamati inakubaliana na marekebisho hayo yaliyopo kwenye muswada huo.

Ameshauri serikali iimarishe Mifumo ya TEHAMA ili wanachama wapate taarifa za michango yao kutoka kwa waajiri kila mwezi kwenye simu zao za kiganjani ili kuondoa tatizo la wanachama kutolipwa mafao kwa wakati kutokana na kutopelekwa kwa michango yao kwenye mifuko.
Share To:

Post A Comment: