Zaidi ya shilingi bilioni 14.1 zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo la Makambako Mkoani Njombe kwa kipindi cha miaka mitatu huku mbunge wa jimbo hilo Deo Sanga kupitia kampuni yake ya Jah People akichangia zaidi ya milioni 490.

Fedha hizo zimetekeleza miradi hiyo katika sekta za Afya,Maji,Nishati na Elimu katika kipindi cha  kuanzia 2021/2022 hadi 2023/2024,ambapo bilioni 11 zimetokana na serikali kuu, bilioni 2.1 mapato ya ndani ya Halmashauri na wadau mbalimbali wakiwemo Wananchi, madiwani na Mbunge ikiwa ni bilioni 1.2.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Makambako Keneth Haule katika mkutano wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020-2025 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Haule amesema halmashauri itaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiweo ujenzi wa soko kuu na stand, ambapo amesema mwezi agoust atakuja mhandisi mshauri wa kuona namna ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo.

Aidha Mbunge wa jimbo la Makambako Deo Sanga amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ambayo imeharibiwa kutokana na mvua zilizonyesha huku akitawataka wataalamu wa halmashauri kuhakikisha wanasimamia fedha zinazotolewa ili zifanye kazi iliyokusudiwa.

Sambamba na hilo pia ameongezea kuwa zaidi ya shilingi milioni 490 nje ya fedha za mfuko wa jimbo amezitoa mfukoni mwake kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu.

Nao baadhi ya wananchi wa halmashauri ya mji wa Makambako Alex Kitalula,Boniface Sanga na Venance Ngimbudzi  wameiomba serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara kwani nyingi hazipitiki

Naye mwakilishi wa meneja wa wakala wa barabara za vijijini na Mjini TARURA wilaya ya Njombe Sikitu Pella amesema wakala huo umejipanga kufanyia kazi changamoto za barabara katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 ambao umeanza sasa.






Share To:

Post A Comment: