Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Serikali imefuta na kurejesha Serikalini Leseni za Utafiti 45 kati ya 102 zilizopo mkoani Rukwa kutokana na kushindwa kufanyiwa kazi na kukidhi masharti yaliyowekwa.

Waziri Mavunde aliyasema hayo jana Wilayani Sumbawanga,wakati akijibu hoja za uongozi wa wachimbaji mkoani Rukwa ya ombi la kupatiwa maeneo ya uchimbaji katika kikao kilichofanyika kati ya Waziri wa Madini na wadau wa sekta ya madini mkoani Rukwa.

"Mhe. Rais Dkt. Samia  Hassan ametupa maelekezo bayana ya kuhakikisha Leseni zinatolewa zinafanya kazi na watu wasihodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi ili kuchochea shughuli za uchimbaji na ukuaji wa sekta ya madini,"

"Mkoani Rukwa Leseni 45 zimerejeshwa Serikalini ili kutoa fursa kwa Serikali kuyapanga vyema maeneo hayo kwa kutenga Leseni kwa ajili ya wachimbaji wadogo na wawekezaji wakubwa walio tayari kuwekeza kwenye sekta ya madini,"

"Hizi leseni 45 tu zilikuwa zimeshikilia eneo kubwa la ekari 812,383 ambalo ni kunwa kuliko eneo la Wilaya nzima ya Sumbawanga ambayo ina eneo la ukubwa wa ekari 667,641,

Alisema uchimbaji hapa mkoani Rukwa upo chini ,hivyo ni jukumu la Ofisi ya Afisa Madini Mkoa kuhakikisha inachochea shughuli za uchimbaji mkoani humo.

Naye, Afisa Madini wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Joseph Kumburu amehakikishia Waziri Mavunde kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo hasa la kuchochea shughuli za uchimbaji wa madini mkoani hapa kwa kuwa Rukwa imejaaliwa madini mengi ya aina tofauti tofauti na hivyo ina fursa kubwa ya kufanya vizuri zaidi.

Akiwasilisha taarifa ya wachimbaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Mkoani Rukwa(RUREMA) Bw. Masie Mwambegele aliiomba Serikali kuwapatia maeneo wachimbaji wadogo katika maeneo ambayo hayafanyiwi kazi na kuomba Serikali iongeze nguvu kwenye eneo la utafiti.

Share To:

Post A Comment: