Na Mwandishi wetu - Zambia


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewasili nchini Zambia leo Julai 21,2024 kwa ajili ya kushiriki mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Utalii wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika (67 CAF) utakaofanyika  sambamba na mkutano wa pili wa kikanda wa Brand Africa jijini Livingstone Zambia kuanzia tarehe 22 hadi 24 Julai 2024.

Waziri Kairuki mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka - Zambia, amepokelewa na mwenyeji wake Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule.

Pamoja na mambo mengine mkutano  huo utajadili mikakati ya kukuza na kutangaza  utalii wa Bara la Afrika na mikakati madhubuti ya mawasiliano ili kujenga taswira  nzuri ya Bara hilo, kujenga upya imani ya soko la utalii na kufufua sekta ya utalii ya Afrika hasa baada ya janga la UVIKO-19.

Waziri Kairuki ameongozana  na ujumbe kutoka nchini Tanzania ukijumuisha Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) , Bw. Ephraim Mafuru, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Richie Wandwi pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bodi ya Utalii Tanzania.

Mkutano huo wenye kaulimbiu inayosisitiza kuhusu kufungua uwekezaji wa utalii na uwezo wa ukuaji wa sekta hiyo “Promoting Africa to unlock tourism investments and the sector’s growth potential” unahudhuriwa na nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, wataalamu katika Sekta ya Utalii, wawakilishi wa taasisi za fedha na huduma za kifedha na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi wanaosimamia na kuendeleza mabadiliko chanya katika Sekta ya Utalii  Barani Afrika.

Share To:

Post A Comment: