Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amehamasisha Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika Sekta ya Misitu, Nyuki na Utalii ili kujiongezea kipato na kupata ajira.
Ameyasema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
“Tunawakaribisha Watanzania kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kuna fursa mbalimbali, kwa wanaotaka kuanzisha biashara za utalii Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB) na Idara ya Utalii ipo kwa ajili ya kuwasaidia ili mjue taratibu zinazoweza kufuatwa” Mhe. Kairuki amesema.
Aidha, amewahamasisha wananchi kujiingiza katika shughuli za ufugaji nyuki ili kujiongezea vipato akitolea mfano wa mwanakikundi kutoka Tabora anayeingiza zaidi ya chini ya Sh. Mil.1 kwa mwezi kutokana na shughuli za ufugaji nyuki.
“Niwakaribishe vijana ambao hawana ajira kuchangamkia fursa kupitia mfuko wetu wa misitu wa TaFF kuomba fursa mbalimbali” amesema.
" Pia njooni mtembelee banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambapo mtaelekezwa fursa lukuki zilizopo, Chuo chetu cha Mafunzo ya Nyuki cha Tabora nao wako tayari kukusaidia wewe ambaye umehitimu mafunzo ya ufugaji nyuki na uchakataji wa asali au hata kama hukusomea mafunzo ya ufugaji “ Waziri Kairuki amesisitiza.
Ametoa rai kwa Wazazi wenye wanafunzi waliohitimu kidato cha nne kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na kuzungumza na wataalamu katika vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama Chuo cha Misitu Olmotonyi, Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na vyuo vingine ili kujua fursa mbalimbali za kujiunga na vyuo hivyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amesema kwa mwaka huu Wizara ya Maliasili na Utalii katika banda la Ngorongoro imeweka kivutio kipya cha Virtual Reality ambapo wananchi wanaona moja kwa moja kinachoendelea katika Hifadhi ya Ngorongoro na watapata fursa nzuri ya kujua Ngorongoro ni kreta ya aina gani na nini kilitokea na kwa nini ni kivutio cha utalii.
Pia, amehamasisha Watanzania kutembelea banda la Wizara kupata mafunzo ya uhifadhi na hifadhi mbalimbali kupitia taasisi mbalimbali za Wizara pamoja na kujionea wanyamapori hai kama Simba, Twiga na wengine wengi.
Waziri Kairuki amewapongeza wadau wa sekta binafsi ambao katika maonesho hayo wanaonesha mambo mbalimbali ikiwemo punguzo la bei kwa biashara zao ikiwemo gharama nafuu za kutembelea hifadhi na huduma zilizopo kwa mfano wa Tanzania Smile Safaris na Serena Hotel.
Waziri Kairuki ameweka bayana kuwa katika banda la Wizara hiyo, Watanzania wataweza kujionea nishati safi za kupikia ukizingatia kwamba, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akitolea mfano wa majiko yanayotumia umeme mdogo
Aidha, Mhe.Kairuki ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa katika banda hilo ndio sehemu pekee wanayoweza kupata bidhaa za asali zisizochakachuliwa.
Post A Comment: