Wananchi zaidi ya 41,168 wa vijiji sita kata ya Akheri Wilayani Arumeru Mkoani Arusha wameanza kunufaika na mradi wa maji safi baada ya wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kusambaza huduma hiyo.

Akisoma taarifa mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mnzava, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Arumeru, Injinia Shabir Waziri amesema mradi huo umegharimu sh. bilioni 1.563 .

Injinia Shabir amesema wananchi hao watanufaika na mradi huo wa maji uliofikia asilimia 95 ya utekelezaji wake na kuongeza kuwa ujenzi  ulianza Aprili 16,2022 na unatarajiwa kukamilika Septemba 30,2024.

Amesema kazi za mradi huo zilizotekelezeka ni ujenzi wa vyanzo vya maji vya mto Malala, ujenzi wa matenki matatu yenye mita za ujazo 500,135 na 50, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba umbali wa mita 48,172 na ujenzi wa ofisi.

Kwa upande wake Mnzava amewaomba wananchi hao kulinda vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibufu badala yake miundombinu ya maji hayo itunzwe

“Lindeni vyanzo vya maji kwani Rais Dkt Samia Hassan Suluhu amedhamiria kutua akinamama ndoo kichwani hivyo miundombinu hii itunzwe kwa manufaa yenu,” amesema Mnzava.

Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, John Palangyo ameishukuru serikali kupeleka maji kwa wananchi hao ambao awali walikuwa wakikabiliwa na adha kubwa ya maji.

Kwa mujibu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini utekelezaji wa miradi Mwaka wa Fedha 2023/2024 katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wakala ulipanga kutekeleza jumla ya Miradi 1,546 katika mikoa 25 nchini, inayogharimu Tshs 500,342,398,033.25.

Miradi hiyo inategemewa kuhudumia watu wapatao 2,274,193 katika vijiji 844.

Katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2023/2024, hadi kufikia Desemba 31, 2023 jumla ya miradi 374 iliyogharimu  Tshs 128,177,655,882 ilikuwa imekamilika.

RUWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi 1,172 iliyobakia ili kutimiza adhma ya serikali ya kutoa huduma ya uhakika ya Maji Safi na Salama vijijini.


Share To:

Post A Comment: