Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema limejipanga kuendana na kauli mbiu ya Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya "Tanzania ni mahali sahihi pa Biashara na Uwekezaji kwa kufungua milango ya kidigitali kwa wawekezaji na Wafanyabiashara ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi Zaidi.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania Bi. Zuhura Muro alipotembelea Banda la Maonesho la Shirika hilo kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Temeke Jijini Dar es Salaam.



Bi. Zuhura amesema shirika hilo linao wajibu mkubwa wa kuunganisha Mawasiliano nchini na mipaka ya nje nchi lengo likiwa ni kurahisisha biashara na kufanya utekelezaji wa majukumu kwa wawekezaji kufanyika kwa urahisi na ubora unaotakiwa.


Amesema TTCL kwa muda sasa imekuwa ikifungua milango ya kidigitali na nchi karibu zote zinazopakana na Tanzania kwakuunganisha nchi hizo kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasliano hivyo bado shirika linalo jukumu la kuunganisha Dunia kidigital kutokana na ubora wa mawasiliano yanayotolewa na shirika hilo.


"Sisi kama TTCL tunafungua milango ya kidigitali na nchi zinazotuzunguka hivyo tunao mkakati wa kuunganisha Tanzania na Dunia kidigitali kutokana na ubora wa Mawasiliano tulionao,"amesema Muro


Amesema pia TTCL ipo tayari kufanya ushirikiano na wawekezaji kwa lengo la kupata huduma nzuri ya Mawasiliano na hivyo kuzikaribisha Taasisi, Makampuni na Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara na shirika hilo kutokana na ukweli kuwa huduma zinazotolewa ni za uhakika na salama.


“Tunazikarbisha Kampuni na Wafanyabiashara kushirikiana nasi kwani tunaamini ushirikiano huo utawawezesha wawekezaji kufanya shughuli zao mbalimbali ikiwemo ya kibiashara kwa kutumia Mawasiliano yetu"amesema


Amesema TTCL imekuwa ikiendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo Shirika limejipanga kuendesha Biashara kila sehemu ikiwemo maeneo ya utalii ili kuunga mkono juhudi za kukuza sekta ya utalii nchini kwakuweka mawasiliano ya Intaneti ili kuyaongezea thamani maeneo hayo ya kitalii.

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: