Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika 2025, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU,) kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 imejipanga kikamilifu kukabiliana na vitendo vyoyote vya rushwa kwa kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi kabla ya kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kufanya uchunguzi na kuendesha mashtaka.
Tayari Taasisi hiyo imekutana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Dini, wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini pamoja na wadau wa Asasi za kiraia (AZAKI,) na Asasi zisizo za Kiserikali (AZIZE,) na kujadili namna ya kudhibiti vitendo vya rushwa katika chaguzi zinazokuja.
Kwa wadau wa AZAKI na AZIZE; Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP. Salum Rashid Hamduni akizungumza na wadau hao alieleza kuwa kutokana na athari zinazoweza kusababishwa na Rushwa katika uchaguzi TAKUKURU imeona ni busara kukutana na viongozi hao wa kwa lengo la kujadili tatizo la rushwa katika uchaguzi, madhara yake na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kupambana na Rushwa kabla madhara hayajatokea.
“TAKUKURU pekee haiwezi kutekeleza jukumu hili la Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Tunatambua kuwa Asasi za Kiraia zimekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na usawa pamoja na kuhamasisha wananchi kutambua wajibu wao katika masuala mbalimbali ya kijamii, uchumi na siasa ikiwemo kushiriki uchaguzi na shughuli za maendeleo…Kwa ukaribu wenu na jamii tunaamini mchango wenu katika kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi.Tumieni mitandao na majukwaa yenu kuelimisha jamii juu ya madhara ya rushwa.”
Kuhusiana na madhara ya rushwa wakati wa uchaguzi CP. Hamduni alieleza ni pamoja na upatikanaji wa viongozi wasio waadilifu, wanaojihusisha na vitendo vya Rushwa pamoja na kutozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo mambo ambayo ni muhimu katika ustawi wa wananchi.” Alieleza.
“La kusikitisha zaidi Rushwa wakati wa uchaguzi hudhalilisha utu kwa kufananisha thamani ya mtu na hongo anayopewa ili apige au asipige kura pia rushwa wakati wa uchaguzi husababisha uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya kisiasa, kusababisha Taifa kuendelea kugubikwa na rushwa, wananchi kutokuwa na imani na Serikali pamoja na kudhoofisha utawala bora na demokrasia kwa wananchi wenye sifa za uongozi bora kushindwa kugombea au kutoteuliwa kwa kutokuwa tayari kutoa hongo.”
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO,) Dkt.Lilian Badi akichangia mada wakati wa mjadala huo alieleza kuwa TAKUKURU imekuwa ikishirikiana na Asasi za kiraia katika mapambano ya rushwa na kueleza kuwa kuelekea wakati wa uchaguzi ni vyema Asasi hizo zikapewa vibali ili ziweze kutoa elimu kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ili kuleta matokeo chanya dhidi ya mapambano ya rushwa.
Dkt. Lilian alieleza ushirikishwaji wa wadau hao ni muhimu kwa kuwa Asasi za Kiraia huwafikia wananchi katika ngazi zote na kuwahudumia katika sekta mbalimbali hivyo kupitia mitandao na majukwaa elimu na hamasa ya kuepuka vitendo vya rushwa itawafikia wananchi kwa kiasi kikubwa.
Lilian Liundi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) alisema mtandao huo umekuwa ukipigania nafasi za ushiriki wa wanawake katika uongozi na kupitia warsha hiyo watajadili vikwazo na kuona namna ya kutoa elimu na kuripoti changamoto katika uchaguzi ikiwemo rushwa ya ngono kwa wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa viongozi wa dini; Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bi. Neema Mwakalyelye akifungua warsha hiyo alieleza; Kikatiba Serikali haina dini ila inatambua wananchi wana dini na vitabu vyote vya dini vina makatazo na kuitambua rushwa kama tendo ovu.
"Katika mapambano dhidi ya rushwa Taasisi pekee haiwezi kufikia Umma wa Watanzania wote na tunatambua nguvu na mchango wenu katika kujenga uadilifu kwa watanzania kupitia mafundisho na mihadhara, Tunaamini kupitia kwenu watanzania watafahamu zaidi athari za rushwa na kuepukana nayo kwa kutoa au kupokea."
Kuhusiana na vitendo vya rushwa katika chaguzi zilizopita Bi. Neema alieleza kuwa vitendo vya rushwa vilikuwepo na walipokea taarifa na kuchukua hatua na kutaja vitendo vya rushwa vilivyoripotiwa ni pamoja na baadhi ya wagombea kutoa Fedha, vitu, na chakula huku mkakati wao ukiwa kufika eneo la tukio na kuchukua hatua na zaidi ni kutoa elimu kwa Umma kuhusu viashiria vya rushwa pamoja na kuacha vitendo vya rushwa kwa kutopokea au kuomba rushwa kwa wagombea.
"Tumelenga sana kuwaepusha watanzania wasiingie katika vitendo vya rushwa ili wasijikute katika mgogoro wa kisheria na TAKUKURU kwa sababu lengo letu ni kuona uchaguzi unakuwa huru na haki na viongozi wanachaguliwa kutokana na uwezo wao wa kuongoza na sio rasilimali walizonazo kwa kuwa tunahitaji viongozi waadilifu na wazalendo mustakabali wa maendeleo ya Taifa."
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT,) Dkt. Alex Malasusa alieleza kuwa kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa dini na TAKUKURU kimelenga kukumbushana wajibu wao katika kuzuia, kupinga na kufundisha athari za rushwa.
" Ombi kwa watanzania wenzangu tukatae rushwa na tumepewa Mamlaka na TAKUKURU ya kutoa taarifa ya nani kapokea au katoa rushwa ili tupate viongozi ambao Mungu amewatayarisha na sio fedha au jambo lolote limewatayarisha kuwa katika uongozi....Kama mjuavyo katika misaafu yote inakataza kula rushwa na sisi kama viongozi wa dini tunaishukuru sana Taasisi hii kwa kutukusanya pamoja na kukumbushana kuhusu jambo hili."
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania Sheikh. Dkt. Alhad Juma Salum alieleza viongozi wa dini wapo pamoja katika kufikisha ajenda hiyo kwa wananchi ili kushirikiana katika kupambana na kuziba mianya ya rushwa na kuhakikisha haina nafasi katika jamii kwa kuwapa mafundisho ya kidini na hofu ya Mungu.
Kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini, CP. Hamduni alieleza kuwa vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na usawa, kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutambua haki na wajibu wao katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ikiwamo kushiriki katika uchaguzi pamoja na shughuli za maendeleo, hivyo vinavyo nafasi ya kusaidia vita dhidi ya rushwa.
“Ukaribu huu mlionao kwa jamii unawafanya kuwa kundi muhimu sana ambalo linaweza kusaidia kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi.
“TAKUKURU inaamini ushiriki wenu katika kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo ya rushwa kwenye uchaguzi una faida kubwa, ikiwamo kuchaguliwa kwa viongozi bora watakaoongoza kwa mujibu wa sheria na kutekeleza mipango ya maendeleo,”alisema.
Mgaya Kingoba Mhariri wa Gazeti la Habari Leo akizungumza wakati wa kikao hicho alivitaka vyombo vya habari kufichua vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi kupitia kalamu na sauti zao kwa kuwa vina nafasi kubwa katika kusaidia uchaguzi na kuhakikisha haugubikwi na vitendo vya rushwa.
Jitihada za Serikali za kudhibiti Rushwa katika uchaguzi Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaendelea ambapo mpaka sasa imechukua hatua mbali mbali za kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki na usiogubikwa
na vitendo vya Rushwa, hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na: Kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchagazi (INEC,) Kutunga Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani, 2024,Kutunga kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024, Kuendelea na maboresho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 pamoja na Kuiwezesha zaidi TAKUKURU ili, kwa kushirikiana na wadau wengine iweze kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi.
Post A Comment: