Kama umekuwa ukifuatilia kwa karibu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kuwezesha ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa Madini ni vizuri kuona matokeo chanya yanayopatikana kupitia hatua mbalimbali kuanzia Marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka 2017 ambayo yalijumuisha hitaji la matumizi ya huduma na bidhaa zinazopatikana nchini Tanzania.

Marekebisho haya yalipelekea kutungwa kwa Kanuni za ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini za Mwaka 2018.

Matokeo ya utekelezwaji wa Kanuni hizo hadi sasa yameonesha dalili nzuri za maendeleo katika eneo hili muhimu la uchumi kwani idadi ya watanzania wanaotoa huduma na kuuza bidhaa kuanzia migodi ya uchimbaji mdogo, Kati hadi uchimbaji mkubwa unazidi kuongezeka.

Dalili hizi zinadhihirishwa na namna ushiriki wa watanzania ulivyoongezeka kupitia takwimu mbalimbali ikiwemo za mwaka 2023 zinazoonesha namna kampuni za kitanzania zilivyouza bidhaa na huduma migodini zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.48 ambayo ni sawa na asilimia 90 ya mauzo yote yaliyofanyika migodini yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.65. 

Aidha, mauzo hayo yaliyofanywa na kampuni za kitanzania kwa mwaka 2023 yalikuwa ni zaidi ya mauzo yaliyofanywa Mwaka 2022 ambayo yalikuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.08 sawa na asilimia 86 ya mauzo yote ya Dola za Marekani bilioni 1.26.

Katika kuendelea kuimarisha huduma hizi kutokana na mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji katika Sekta ya Madini, tayari kampuni tatu (3) za kitanzania zimejenga viwanda vya kutengeneza vifaa vinavyotumika migodini katika eneo la Buzwagi Special Economic Zone. 

Kampuni hizo ni East African Conveyors Supplies Limited imejenga kiwanda cha kuzalisha conveyor belts zinazotumika kusafirisha miamba wakati wa uchakataji wa madini kilichopo Manispaa ya Kahama ambapo ujenzi wake umekamilika na tayari  kimeanza usambazaji wa bidhaa hizo katika migodi ya ndani na nje ya nchi. Pia, Kampuni ya Max Steel Limited iliyopo jijini Dar es Salaam inatarajia kuzalisha vifaa vinavyotumika kushikilia miamba (wire-mesh na rock-bolts) kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 90.

Vilevile, Kampuni ya Rock Solutions Limited inajenga kiwanda jijini Mwanza cha kuzalisha core-trays zinazotumika kutunzia sampuli za miamba iliyochorongwa ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 90. Aidha, tayari kuna kampuni 8 zimeonesha nia ya kujenga viwanda vya uzalishaji bidhaa hizi.

Kwa Serikali haya ni mafanikio makubwa na ndiyo sababu Wizara inaendelea kuhamasisha watanzania na wadau wengine kuchangamkia fursa hizo za uwekezaji kupitia eneo la utoaji huduma migodini.  

Kwa upande wa Wizara imeendelea kukutana na kujadili kwa pamoja na wadau kupitia majukwaa maalum kwa lengo la kuendelea kuboresha zaidi eneo hilo kwani kupitia uwekezaji huo, taifa litaendelea kupiga hatua kubwa za kiuchumi kupitia Sekta ya Madini.

Hivyo, kupitia makala hii, watanzania na wadau wengine wanahamasishwa kuchangamkia fursa ya kuanzisha viwanda vya kuzalisha vifaa pamoja na bidhaa mbalimbali zinazotumika migodini ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Dhamira ya Serikali ni kuona Tanzania inakua kinara duniani kwa kuzalisha bidhaa za migodini zinazokidhi mahitaji na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha bidhaa za migodini.

Vilevile, bado  kuna fursa tele katika eneo la utoaji huduma migodini kutokana na migodi mikubwa na ya kati ambayo iko mbioni kuanzishwa katika miaka ya karibuni katika maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania.

Serikali   kwa upande wake inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini na ndiyo sababu inaendelea kuvutia wawekezaji zaidi hivyo, jukumu la kuona fursa hizi na kuzitumia ni la watanzania. Aidha, matokeo haya hayajatokea tu bali kupitia juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya kuifanya Tanzania kitovu cha madini duniani.

VISION 2030: MadininiMaisha&Utajiri

                                                    InvestInTanzaniaMiningSector





Share To:

Post A Comment: