Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetibu vikwazo vya miradi mbalimbali mkoani Njombe ambapo ameridhia kuanza kwa mradi wa Mchuchuma na Liganga kwa kutoa shilingi Bilioni 15 kulipa fidia pamoja na kukubali kuanza kwa mradi mkubwa wa chuma wa Maganga - Matitu akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi.


Vikwazo vingine vilivyotibiwa ni pamoja na kuimarisha na kujenga miundombinu ya barabara ikiwemo kutoa jumla ya shilingi Bilioni 120.9 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Itoni -Ludewa - Manda kipande cha Itoni - Lusitu kwa kiwango cha zege ambayo ni barabara yenye gharama kubwa kuliko zote Tanzania.


"Dhamira ya Mhe. Rais kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha zege ndani ya muda kama ilivyokusudiwa, Pesa zipo wakandarasi wapo, tulipata changamoto ya mvua lakini kwa sasa miradi inaendelea na wananchi waanze kufuatilia fursa za uwekezaji zitakazoimarisha uchumi wao" Amesema Rc Mtaka


Akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalua amesema kuwa Mkataba wa Ujenzi wa Barabara hii ulitiwa saini kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkandarasi M\/s China Civil Engineering Construction Cooperation kutoka China tarehe 29 Machi, 2022 kwa gharama ya Shilingi  Bilioni 120.9 pamoja na VAT.

Share To:

Post A Comment: