RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Jakaya Kikwete ameongoza maelfu ya wananchi wakiwemo wanariadha wa timu ya Taifa kushiriki katika Msoga Marathon iliyoandaliwa kwa ajili ya kuchangisha fedha ili kupata fedha kuboresha huduma ya afya ya mama na Mtoto.


Washiriki katika Marathon hiyo wamekimbia umbali wa kilometa 21,kilometa 10 pamoja na kilometa Tano ambapo washindi mbali ya kupokea medali wameondoka na fedha ambazo zimetolewa kama motisha kwao.

Katika Marathon hiyo iliyonogeshwa na burudani za nyimbo mbalimbali zilizokuwa zikiimbwa na Klabu mbalimbali zinazojihusisha na mazoezi ya viungo yanayoambana na ukimbiaji, zilianza na kumalizikia katika Viwanja vya Msoga Wilayani Chalinze.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi kwa washindi wa Marathon hiyo,Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amewashukuru wote walioshiriki mbio hizo na kwamba mwakani zitakuwa bora zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka huu ambao ndio wameanza .

"Binafsi nashukuru kwa kualikwa na kushirikishwa katika jambo hili jema ,nilishazungumza wakati wa kuzindua mbio hizi.Leo niwashukuru wote kwa kujitokeza kwa wingi .Niliposema wakati ule sikuamini kama watu watakuwa wengi kiasi hiki, muitikio ni mkubwa sana tofauti na tulivyotarajia.

"Nawashukuru kwa kujitokeza , nawashukuru kwa kuchangia na niwapongeze waliobuni kwa kuwa na mbio hizi.Matumaini yangu kama utaratibu huu utaendelea mbio zijazo zitakuwa bora zaidi.

"Nawapongeza sana kwasababu wengi walioshinda wako timu yetu ya Taifa na hapa Chalinze tunavyovilima vikali kwa ajili ya mazoezi hivyo vijana Wetu wa timu ya Taifa tunawakaribisha na mtakapoamua kuweka kambi ya mazoezi nami nitasaidia,"amesema Rais Mstaafu Kikwete.

Awali Mbunge wa Jimbo la Chalinze ambaye pia ni Naibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwan Kikwete amesema lengo la kuandaliwa kwa Marathon hiyo ni kuendeleza na kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka nguvu kubwa kuboresha afya ya mama na Mtoto.

"Tuliona tuanzishe ili Serikali ije ituunge mkono na uamuzi wa kuja na marathon hii ni ukweli kwamba katika maisha haya Serikali peke yake haiwezi kuleta maendeleo kama watu ambavyo wanafikiria.

"Viongozi tulikutana tukaja na wazo hili la kuwa na Marathon kwa ajili ya kupata fedha tuboreshe huduma ya mama na mwanaye na lengo ilikuwa ni kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watoto na akina mama wanaendelea kukaa katika mazingira mazuri,"amesema.

Pia amesema Rais Samia ameendelea kuboresha miundombinu katika sekta ya afya huku akisisitiza viongozi wa Chalinze pamoja na wananchi sekta ya afya wameipa kipaumbele na Hospitali ya Wilaya ya Chalinze imeboreshwa kwani ilianza kama Kituo cha afya baada kuondokewa shule iliyokuwepo eneo hilo.

"Rais mstaafu na baba mlezi wa Serikali hii na Chalinze yetu tunakushukuru kwa ushauri na hata pale ambapo mambo yalikuwa hajajakaa ulitushauri na leo tumefanikisha marathon hii kwa ajili ya afya ya mama na mtoto."

Ridhiwani amesema wanaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Samia na wamefanya hivyo katika maeneo mengi.
"Tumehakikisha hospitali yetu ya Wilaya inajengwa , hospitali hii ya Wilaya ambayo mwanzoni ilikuwa Shule ya Msingi ambayo Rais mstaafu Kikwete akisoma hapo.

"Tulipokuja na wazo Shule ibomolewe ili tujenge wewe mlipokaa na wenzako hamkusita kutukubalia .Hospitali ilianza kama kituo cha afya na leo tunafurahi hospitali yetu imekamilika,"amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuzishukuru joging zote na makundi ya Whatsapp ambao wamefika kwenye Marathon hizo ambazo zinazolenga kusaidia afya ya mama na mtoto.

Kwa upande wake Grace Ndesario Shuna mkazi wa Chalinze amepata zawadi ya fedha kwa kuwa mmoja ya wakimbiaji mwenye umri wa miaka 60 lakini amefanikiwa kukimbia kilometa 10.

"Nimezaliwa mwaka 1964, kiukweli maisha yangu ni ya kawaida lakini napenda kucheza na kukimbia.Nimeshiriki Marathon hii kwasababu ya kuchangia afya ya mama na mtoto,nilikuwa na binti aliyekuwa amezaa mtoto njiti na nilikuwa naona anavyopata shida kumuweka mtoto kifuani apate joto la mama."













Share To:

Post A Comment: