Mshauri wa Ubora wa Huduma za Afya Mradi wa Afya Hatua THPS Makao Makuu, Agnes Kirato (kulia) akimwelezea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha kuhusu huduma za afya zinazotolewa na THPS.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Asasi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Health Promotion Support (THPS) imeendelea kutoa elimu na huduma za kupima VVU, afua za kinga, uchunguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi  na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye maadhimisho ya siku ya Afya Duniani ambayo katika Mkoa wa Shinyanga  yanafanyika kwenye uwanja wa CCM Kambarage.

Maadhimisho hayo yanafanyika kupitia kampeni ya “Afya yangu, haki yangu” maarufu AFYA CODE CLINIC SHINYANGA na kwamba  yanafanyika kwa siku nne ambapo yatahitimishwa Jumamosi Julai 27 Mwaka huu 2024.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha pamoja na mambo mengine leo ametembelea banda la THPS na kupongeza kwa huduma hizo zinazolenga kutatua changamoto za kiafya kwa wananchi.

"Kwanza niwapongeze kwa kazi kubwa mnayofanya na sisi tunawashukuru , ni vizuri kuwa na maeneo kama haya kwa maana ya kwamba tunataka watu wakimbilie kwenye maeneo yanayotoa elimu kwa sababu elimu ndiyo tiba ya kwanza halafu kupima ni tiba ya pili halafu inayofuata kushauriwa ya tatu ni matibabu. Kama watu wangetumia muda mwingi kupata elimu mambo mengi tungeweza kuyaepuka",amesema Mhe. Macha.

"Nimeona THPS mnafanya huduma ya Tohara Kinga kwa wanaume,Ndugu zangu Tohara Kinga siyo jambo la siri wananchi jitokezeni kupata tohara Kinga",amesema Mhe. Macha.

Kupitia mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia kituo cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa cha Marekani ( CDC), Tanzania Health Promotion Support (THPS) inashiriki katika maadhimisho hayo kwa kutoa elimu na huduma za Afya kwa wakazi wa Shinyanga.

Meneja mradi wa THPS Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Amos Scott ametumia nafasi hiyo kutaja mafanikio ya asasi hiyo ambapo amesema kwa kipindi cha Mwezi Oktoba 2023 hadi Juni 2024 jumla ya wapokea huduma 21,759 walipimwa Saratani ya mlango wa kizazi ambapo 563 waligundulika kuwa na viashiria vya Saratani hiyo na 552 kati yao walipatiwa matibabu.

“Tunaendelea kuwaokoa akina mama dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, Tunaomba wanawake wajenge tabia ya kupima afya zao kwani saratani nyingi zikiweza kufanyiwa uchunguzi wa awali zinatibika, isipotibiwa mapema ni ngumu kutibiwa”,amesema Dkt. Scott.

DKT. Scott amesema THPS imeendelea kutoa huduma za Afya mahususi kwa vijana na kwamba hadi kufikia mwishoni mwa Mwezi Juni 2024, mradi wa Afya Hatua umetoa huduma kwa vijana 4,027 wanaoishi na VVU ambapo 3,082 ni wanawake na 1,125 na wanaume huku akieleza kuwa THPS inafanya kazi na vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya ili kuhakikisha matumizi sahihi ya dawa za kufubaza VVU kwa wapokea huduma.

THPS inafanya kazi kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar; Wizara ya jinsia, vijana, wazee, na makundi maalum; ofisi ya Rais, tawala za Mikoa na serikali za mitaa na Wizara ya mambo ya ndani ya nchi.

Kwa ufadhili wa mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia kituo cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa (U.S. CDC), THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU\UKIMWI; kifua kikuu; kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto; huduma za Afya ya uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana; mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa Afya na UVIKO – 19.

Aidha kuhusu mradi wa CDC\PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021 – Septemba, 2026) mradi huo unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya Afya ukiwemo Mkoa wa Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga.

Pia huduma hizo ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika Mikoa ya Kigoma na Shinyanga na program ya DREAMS kwa wanawake katika Mkoa wa Shinyanga.

Wakizungumza baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wameishukuru asasi ya THPS kwa huduma nzuri na kwamba zimesababisha kufahamu hali zao za kiafya huku wakiahidi kuzingatia maelekezo waliyopewa kwa lengo la kuimarisha Afya zao. 


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akiwapongeza watumishi wa  THPS kwa kuendelea kutoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akiwapongeza watumishi wa  THPS kwa kuendelea kutoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu.

TAZAMA VIDEO

 

Share To:

Misalaba

Post A Comment: