Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru 2024 Ndugu Godfrey Mnzava amezitaka Halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha vikundi vya vijana vinavyofanya vizuri kwenye miradi ikiwemo ya ufugaji vipewe vipaumbele kupitia mikopo ya asilimia kumi inayotolewa halmashauri.

Akizungumza wakati alipotembelea mradi wa uwezeshaji vijana kikundi cha Iloonyok kata ya Engikaret Wilayani Longido,Kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa, Godfrey Mnzava aliagiza halmshauri zote nchini kuwapa kipaumbele kwenye mikopo ya asilimia kumi  vijana wanaofanya vizuri katika miradi mbalimbali waliyobuni.

"Vijana wanaofanya vizuri kwenye miradi wapewe vipaumbele vya kupata mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri kwani wanaonyesha bidii katika urejeshwaji wake"

Alisisitiza vijana hao kuendelea kukopeshana kama faida ya mikopo kutokana na aina ya ufugaji wa mifugo wanayonenepesha na kuuza kisha faida wanayopata wakitumia kukopeshana bati kwaaajili ya ujenzi wa nyumba za kisasa

Naye Katibu wa Kikundi hicho,Looyani Kiliani akisoma taarifa ya kikundi hicho alisema  lengo lao ni kukuza mtaji na kuimarisha uchumi kwa makundi ya vijana kwani mradi huo ulianza na sh,milioni 4 zilizotokana na fedha za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwaaajili ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Alisema awali walianza kununua mbuzi 10,kondoo 20 ,ndama mmoja pamoja na chakula na madawa kwa lengo la kunenepesha na kuuza kwa faida  ambao mradi huo uliwawezesha kukuza mtaji kwa kuongeza idadi ya mifugo kutoka mbuzi na kondoo 30 hadi kufikia 40 ikiwemo kurejesha marejesho ya mkopo

Alisema kikundi hicho kinatarajia kuimarisha hali ya makazi kwa wanachama wake kwa kutenga kiasi cha sh ,30,000 kwa kila wanachama kwaaajili ya ununuzi wa bati za ujenzi kutokana na faida wanayoipata baada ya uuzaji wa mifugo mwaka huu

Aliishukuru serikali chini ya uongozi wa Rais,Samia Hassan Suluhu kwa utoaji wa mikopo ya asilimia kumi inayowasaidia kuwa na mradi huo unaowasaidia kuboresha uchumi.

Mwenge huo ukiwa wilayani Longido  ulipitia miradi nane yenye thamani ya sh,bilioni 6.4 ambapo mradi moja iliwekwa jiwe la msingi,miradi mitano ilitembelewa huku miradi miwili ikizinduliwa

Awali Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda  akikabidhi mwenge huo wilayani Longido ulitokea wilayani Arumeru,alishukuru kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana naye pamoja na watumishi  wengine akiwemo Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Arusha Vijijini, Suleiman Msumi ambao kwa pamoja waliwezesha miradi hiyo kuzinduliwa na mingine kuwekwa mawe ya msingi na kiongozi huyo wa mbio za mwenge.






Share To:

Post A Comment: