Wizara ya Madini imemkabidhi rasmi Mkandarasi Kampuni ya Ujenzi ya Skywards eneo litakapojengwa Jengo la Kisasa la Ghorofa Nane (8) la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Arusha katika Kituo cha TGC na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Madini,  Ashura Urassa kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mratibu wa Kituo hicho Ally Maganga, wataalam kutoka Wizara ya Madini na TGC, Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Arusha Mussa Shanyangi, pamoja na Mshauri Elekezi Kampuni ya Epitome Architects.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Mratibu wa Kituo hicho Ally Maganga amesema kukamilika kwa jengo hilo kunatarajia kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Uongezaji Thamani Madini ya Vito na usonara na kueleza kwamba, TGC imejipanga kutoa elimu itakayokidhi viwango vya kimataifa kutokana na miundombinu muhimu inayotarajiwa kuwekwa katika jengo hilo ikiwemo  ushirikiano ulioanzishwa na taasisi nyingine za kimataifa ambao umelenga kuzalisha watalaam wenye viwango vyenye ubora wa juu.

"Elimu itakayotolewa itakidhi viwango vya kimataifa na kituo hiki kinakwenda kuwa kitovu cha madini ya vito na mnyororo mzima wa shughuli za uongezaji thamani madini ya vito. Tunatarajia baada ya kukamilika watanzania watanufaika pamoja na kuwavutia wanafunzi zaidi kutoka nje ya Tanzania" amesema Maganga

Kituo cha TGC kinatoa mafunzo ya uongezaji thamani madini yakihusisha ukataji, ung"arishaji madini ya vito, utambuzi wa madini, jiolojia na huduma  mbalimbali kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya vito. Aidha, tayari kituo hicho kimepokea wanafunzi kutoka nchi za Kongo na Afrika Kusini wanaoendelea na mafunzo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Wizara ya MadiniAshura Urassa, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini, amemtaka Mkandarasi kufanya kazi kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotolewa pamoja na muda uliowekwa kulingana na mkataba wa ujenzi.












Share To:

Post A Comment: