Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Geita
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amesema lengo la Serikali kutoa ruzuku ya ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini ni kuwaunganisha na kuwasogeza Watanzania na Dunia ya Kidigitali ili wasiachwe nyuma na huduma nyingi, alizosema, zitaendeshwa kidigitali, muda siyo mrefu.
Huduma hizo ni pamoja na uombaji na ulipaji wa pasi za kusafiria, huduma za kutuma na kupokea fedha ndani na nje ya nchi, huduma za afya, biashara ya kimtandao, leseni za magari na nyinginezo.
Waziri Nape ametoa kauli hiyo Julai 17, 2024, wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Luhuha, Kata ya Nyakagomba wilayani Geita na Kijiji cha Busonzo Kata ya Busonzo Wilayani Bukombe, katika Mkoa wa Geita.
"Huko tunakokwenda tunayaendea mabadiliko makubwa sana ya sayansi na teknolojia na matumizi ya TEHAMA, usipoyajua utajikuta umeachwa nyuma na Serikali ya Rais Samia haitaki kumuacha nyuma Mtanzania yeyote," amesema Waziri Nape na kuongeza;
"..huko tuendako baadhi ya hospitali tumeanza kuziunganisha na mtandao, Daktari anaishi Dar es Salaam anamtibu mtu wa Busonzo, unahitaji huduma za passport unajaza fomu na kulipia kidigitali na sasa hivi tuna Anwani za Makazi watu wa Posta wanaweza kukuletea pasi yako ya kusafiria hadi nyumbani."
Amesema minara inayokaguliwa ni sehemu ya mradi wa minara 758 ambayo Serikali inatoa ruzuku kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kusisitiza "niwe mkweli tangu mfuko huu uanzishwe haijawahi kutekelezwa minara mingi kiasi hiki kwa wakati mmoja".
Aidha, Waziri Nape amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela kuzungumza na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ili watoe kipaumbele cha kupeleka huduma za miundombinu ya barabara na umeme kwenye maeneo yote inakojengwa minara ili kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji wake na hivyo wananchi wapate mawasiliano saa 24.
Amesema, mnara mmoja unatumia takribani shilingi milioni 1.8 kwa mwezi kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea jenereta lakini ukipelekwa umeme gharama za uendeshaji zinapungua hadi shilingi 400,000 kwa mwezi.
Post A Comment: