Na. Catherine Sungura, Dodoma


Naibu Katibu Mkuu , Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila amefurahishwa na viwango vya ujenzi wa miradi ya barabara za lami zinazosimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Dodoma.

Mhandisi Mativila ameyasema hayo mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya kukagua uimara wa barabara zinazosimamiwa na TARURA ambapo alitembelea miradi minane.

Alisema barabara zote hizo zimejengwa kwa fedha za tozo na mfuko wa maendeleo wa barabara ambazo hutolewa na serikali kwaajili ya kuboresha miundombinu ya barabara hususani maeneo ya mijini.

“Nimefurahishwa na viwango vya barabara hizi ambazo zinasimamiwa na TARURA pamoja na makandarasi waliojenga barabara mkoani Dodoma, wamefanya kazi nzuri na hata kwa kuangalia kwa macho barabara zote zipo kwenye viwango vizuri hata wakazi wanaoishi jirani na barabara hizi unaona wanavyofurahia barabara hizi.”


Aliongeza kusema kwamba anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwaajili ya kuboresha miundombinu ya barabara hususani barabara za mijini.

"Sisi tunashukuru sana kwa kutupa maisha bora kupitia miundombinu ambayo Mhe. Rais aliamua kuongeza fedha na kuhakikisha zinajengwa barabara kwa kiwango cha lami".Aliongeza Mha. Mativila

Aidha, akiwa kwenye barababa inayounganisha barabara ya kutoka Dodoma kwenda Singida (Nala) inayoelekea kiwanda cha mbolea cha Itracom Fertilizer Limited yenye urefu wa Km. 5, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kwenye sera ya viwanda zipo fedha ambazo serikali imeongeza fedha za tozo ambazo zinatumika katika maendeleo ya miundombinu inayoenda kwenye viwanda ambapo viwanda hivyo vinatoa ajira kwa watanzania pia kwa mbolea inayotengenezwa hapo inauzwa kwa bei nafuu.

"Barabara hii inasaidia kiuchumi na kijamii kwani maeneo jirani na kiwanda hiki yamepimwa hivyo inawarahisishia usafiri pia wakazi wa Dodoma wanapata ajira kupitia kiwanda hiki". Alisisitiza.

Hata hivyo Mha. Mativila alisema barabara hiyo inayoruhusu magari yenye kubeba mizigo yenye uzito wa Tani 56 na hivyo kurahisisha usafirishaji wa malighafi kutoka nje ya kiwanda na pia mbolea toka kiwandani na kuwafikia wananchi kwaajili ya kilimo.

Naye, Msimamizi wa miradi wa barabara ya Swaswa-Mpamaa yenye urefu wa Km. 8.7 Mhandisi Atuletile Ngailo amesema mradi huo umeweza kukuza uchumi wa wakazi hao pia umewapunguzia umbali kwa kutumia barabara hiyo.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA wilaya ya Dodoma Mhandisi Emmanuel Mfinaga alisema barabara zilizojengwa mjini hapa zimekuwa mkombozi kwa wananchi kwani maeneo mengi hayakuwa na barabara kabisa na hivyo ameishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka fedha za kutengeneza na kuboresha barabara wilayani Dodoma.

Bi. Rehema Malongo Mkazi wa Nala alisema wanaishukuru serikali kwa kujenga barabara ya lami kuelekea maeneo ya viwandani kwani imewarahisihia usafiri wa mazao yao na pia vijana wao kupata ajira kupitia kiwanda hicho cha mbolea.



Share To:

Post A Comment: