Na. Catherine Sungura, Mbeya


Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali  za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuwasaidia na  kuwashauri watendaji wafanye kazi vizuri ili kuhakikisha anayoyaota Mhe. Rais kwa Watanzania yanatimia.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi  wa Bodi ya Wakala huo ulofanyika  jijijni Mbeya.

“Mwenyekiti wa bodi tutakuwa na kazi kubwa ya kuwashauri watendaji hawa, niwaombe bodi mtusaidie na kutushauri kwani wananchi wanataka barabara na bajeti ya TARURA imeongezeka kutoka milioni 200 hadi kufika Tilioni  1.3”.

Hata hivyo ameitaka bodi hiyo kuwa wabunifu na kujipanga ili barabara zinazosimamiwa na TARURA kukamilika pia kushirikiana na wataalam kuhakikisha mchakato wa kuanzishwa kwa hati fungani unakamilika na kuzinduliwa ili kuwasaidia wakandarasi wazawa.

Aidha,Waziri Mchengerwa ameipongeza TARURA kwa kazi kubwa walizofanya nchini za ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja licha ya kusombwa na maji wakati wa mafuriko.

“Nimpongeze Mtendaji Mkuu kwa kazi nzuri anayofanya,pongezi hizi zishuke hadi kwa watumishi wa chini  kwani matokeo ya kazi nzuri zinaonekana  kwa wananchi.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kwa Taifa letu bidii na kujitolea inahitajika, tumefanya kazi kubwa na nzuri ila yakaja mafuriko yakasomba barabara na madaraja,kwa sasa hakikisheni tunajenga upya barabara na madaraja “Aliongeza

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Huduma za Jamii Mhe. Justine Nyamoga  alisema  kamati yake itatoa ushirikiano  ili kuleta  tija kwa wananchi na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi. 

Wakati huo huo Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff alisema bodi hiyo ni ya pili tangu kuanzishwa kwa Wakala huo.

Pia jukumu kubwa la Bodi ya Ushauri ni kumshauru Waziri OR-TAMISEMI kwenye mipango ya kimkakati, namna ya kufikia malengo, upangaji wa vipaumbele, mipango ya bajeti,tathimini na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali za utendaji kazi pamoja na maeneo mengine ya TARURA.

Share To:

Post A Comment: