Wananchi wa makundi mbalimbali wilayani Makete mkoani Njombe wametoa maoni yao kuhusu utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo 2025 na matarajio ya dira mpya ya maendeleo ya miaka 25 ijayo yaani 2025-20250.

Wananchi hao wametoa maoni yao katika kikao hicho kilichofanyika Julai 29, 2024 katika Ukumbi wa halmashauri hiyo ambapo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri William Makufwe ameeleza umuhimu wa maoni hayo ili kukamilisha dira hiyo.

Egnatio Mtawa ni Mkurugenzi wa Shirika la SUMASESU na kituo cha Redio Green FM na Mwinjilisti Ayubu Lwilla Mkurugenzi wa asasi iitwayo PACEP wamepata nafasi ya kuchokoza mada katika kikao hicho na kusema dira ni muhimu kwa kizazi cha sasa na cha badaye huku wakiwaonya wanasiasa kuwa makini kwani wananchi wa sasa ni waelewa na wanapenda kuhoji.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho Mchungaji Raphael Sowo na Shedrack Kamage wamesema pamoja na mabadiliko yaliyofanywa na serikali katika dira hii ambayo inaishia 2025, yapo mambo ambayo wangependa serikali iyafanye ikiwemo kila kaya kupata ng’ombe wa maziwa kutoka shamba la mifugo la Kitulo, barabara za kuelekea mashambani ziboreshwe ili kurahisisha mazao kufika sokoni pamoja na wajasiriamali kupatiwa vitambulisho vya ujasiriamali.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda amesema ni wakati wa wilaya kujikita kwenye kilimo cha mazao ya kimkakati pamoja na kukabiliana na udumavu kupitia mifugo itakayozalishwa kwenye shamba la kitulo na wananchi kupata ng’ombe wa kufuga.

Share To:

Post A Comment: