NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ameipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ubunifu na ufanisi katika usimamizi na utatuzi wa changamoto na malalamiko katika sekta ya Habari na Mawasiliano.
Mhandisi Mahundi ametoa pongezi hizo leo Julai 16, 2024 alipotembelea Mamlaka hiyo kwa ajili ya kupitishwa kwenye majukumu yanayotekelezwa na mamlaka hiyo na namna wanavyoshughulikia masuala ya habari na mawasiliano yaliyo chini ya dhamana yao.
Ameongeza kuwa kufanya vizuri kwa Mamlaka hiyo kunaisaidia Wizara lakini pia inaongeza imani ya wananchi kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika ziara yake TCRA, Mhandisi Mahundi amejionea namna mamlaka hiyo inavyohudumia wateja; teknolojia wanazotumia kupima masafa na ubora wa mawasiliano; na ufuatiliaji wa maudhui ya watoa huduma za mawasiliano.
Akizungumzia kuhusu kukua kwa teknolojia ya Habari na Mawasiliano Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Jabir Kuwe amesema matumizi ya teknolojia hiyo yana fursa nyingi za kidijiti lakini pia yana changamoto zake.
Akifafanua hilo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa makini katika matumizi ya teknolojia hiyo na kile wanachochapisha mtandaoni kwasababu kupitia teknolojia taarifa nyingi binafsi huvunwa na kuchakatwa wakati mwingine bila ya mhusika kujua kuwa ameacha alama.
Mhe. Mhandisi Mahundi anafanya ziara ya kikazi ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo pamoja na makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano kwa lengo la kufahamu majukumu wanayotekeleza na namna wanavyowahudumia wateja wao na wananchi kwa ujumla.
Post A Comment: