Kamati za Ulinzi wa wanawake na watoto ngazi ya mitaa na vijiji nchini, zimepewa wiki mbili kuanzia tarehe 01 Agosti, 2024 kuhakikisha zinakaa vikao vya dharura kujadili mbinu za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye maeneo yao na kutoa taarifa.
Maagizo hayo yametolewa Julai 27, 2024 katika kata ya Kibondemaji, Temeke mkoani Dar Es Salaam, wakati wa ziara ya kisekta ya Mawaziri watatu, yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa Kamati za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) ngazi za mitaa na vijiji Julai 27, 2024.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt.Dorothy Gwajima akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa kata ya Kibondemaji amesema Kamati hizo zitapimwa na kutangaza matokeo kwa uwazi.
"Mipango na mikakati imilikiwe na vikao vyote rasmi kuanzia baraza la Kijiji, baraza la maendeleo ya kata, CMT, vikao vya kamati za baraza la madiwani, baraza la madiwani, Baraza la Ushauri la Wilaya (DCC) na Baraza la ushauri la Mkoa (RCC), wajumbe wa kamati watangazwe ili wajulikane na jamii." amehimiza Waziri Gwajima.
Aidha, amewataka viongozi hasa wenyeviti wa Serikali za mitaa kuchagua viongozi wenza kutoka kwa wadau wa maendeleo, sekta binafsi na watu wanaoheshimika na jamii kuwasaidia iwapo watazidiwa na majukumu kuhakikisha kamati hazipitwi na vikao pamoja na kuhakikisha watoto wote wanaelimishwa ndani ya mitaa kama mojawapo ya mkakati kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe.Mhandisi Hamad Masauni amesema ajenda ya ukatili ni muhimu sana kwa sababu inagusa maisha ya Watoto ambao ni tegemeo kwa Taifa hapo baadaye.
"Tukiruhusu hali hii kuendelea tunakuwa hatuwatendei haki. Tulilolifanya leo linaashiria nia ya dhati ya Serikali kunusuru Watoto wetu" Amesema Mhe. Masauni.
Mhe. Masauni amebainisha kuwa, matukio ya ukatili yamepungua kwa ujumla wake kwa asilimia 05 kutoka mwaka 2022 hadi 2024 lakini uhalifu dhidi ya Watoto umeongezeka kutoka 21317 mwaka 2022/23 hadi 24535 mwaka 2023/24.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameitaka jamii kukataa kwa pamoja vitendo vya ukatili kwa kushirikiana kutoa taarifa kuhusu dalili zozote za uhalifu kwenye maeneo yao.
"Jamii yetu sasa ni lazima tuseme basi kwa ukatili wa watoto, tuna kanuni, miongozo, sheria mbalimbali na tuna kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, ni jukumu la watanzania wote kutoa taarifa" amesema Mhe. Pindi.
Baadhi ya wananchi wa Mbagala Kuu na Kibondemaji wamesema wameshaanza kuchukua hatua za kuhakikisha wanatokomeza ukatili hasa kwa watoto, ikiwemo kukaa vikao na kutoa elimu kwenye mikusanyiko mbalimbali huku wakikemea baadhi ya wananchi wanaozusha taarifa za kupotosha na kuzua taharuki.
"Suala la ukatili wa watoto linaanzia nyumbani, wazazi wanawaacha watoto hawawafuatilii. Tufuatilie mienendo ya watoto wetu, wazazi wengine hawana muda na watoto wao" wamesema Salha Omari na Mcheni Khassim.
Hata hivyo, Mawaziri hao wameipongeza Wilaya yaTemeke kwa hatua zilizochukuliwa kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Mitaa katika kuzuia vitendo hivyo kutoendelea huku wananchi wakishukuru jeshi la polisi nchini kwa ushirikiano katika kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.
Ziara hiyo ya kisekta itakayofanyika nchi nzima, inalenga kufuatilia utekelezaji wa Kamati za Ulinzi wa Watoto na Wanawake dhidi ya ukatili na kuelimisha jamii juu ya wajibu wao kwenye vita hivi na ushirikiano wao na Serikali.
Post A Comment: