Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano nchini walio pembezoni wametakiwa kutumia vizuri na kwa faida hususan huduma za kifedha kwani ndiyo benki zao.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 15 Julai, na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye wakati akizungumza na wananchi katika Kata mbili za Wilaya ya Kibondo akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoa wa Kigoma kukagua Miradi ya Ujenzi wa Minara ya Mawasiliano ya simu.
Amesema siyo rahisi huduma za kibenki kufikishwa hadi vijijini lakini Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeona umuhimu wa kuwafikishia minara ya Mawasiliano itakayosaidia pamoja na mambo mengine kuwezesha wananchi kupata huduma za kutunza, kutoa na kutuma fedha kupitia simu.
"Kupitia mnara huu kuna watu hususani vijana watajiajiri, jitafutieni maendeleo, saidianeni kuijenga nchi yetu, kupitia minara hii mtaweza kupokea na kutuma fedha, mtachangia katika uchumi wa kidigitali, sasa tumieni vizuri," amesema Waziri Nape.
Amewataka wananchi pia kutumia vizuri mitandao na kuacha tabia ya kuitumia kutukana viongozi, kufanya utapeli na vitendo vingine kwani mitandao inaacha alama zitakazowaingiza kwenye matatizo.
" Nataka kuwaasa vijana wenzangu, teknolojia inaacha alama katika kila jambo unalolifanya, mtu asikudanganye utafuta utakimbia, havifutiki, itafutika kwenye simu yako lakini huko hewani tutaendelea kuwa nayo, ukitaka usalama daaa yake moja tu wewe tumia mawasiliano kwa haki na usalama, amesisitiza Waziri Nape.
Amesema mawasiliano watakayopata kupitia minara iliyojengwa katika Kata ya Mulungu Kijiji cha Kumbanga na Kijiji cha Bunyambo Kata ya Bunyambo itumike kwa maendeleo na kwa faida zao na siyo kutumia kutukana viongozi, watu wengine wala kutapeli.
Amewatahadhalisha wananchi kuwa macho wasitapeliwe kwani Serikali inawaunganisha kwa mawasiliano kwa lengo la kuwafikishia faida majumbani ikiwemo kuwa na uhakika wa huduma za kifedha, ajira kwa watakaochangamkia na mawasiliano wakati wote.
"Lakini msiwaache watoto wenu wakashinda kutwa kwenye mitandao kwani mitandao ina mambo mabaya na mema, watu wengi wameharibika msishangae watoto wenu wamebadilika tabia mkamlaumu Nape na Rais Samia kwamba wametuletea mnara nimeshawatahadhalisha," amesema
Post A Comment: