Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhakikisha anasimamia ujenzi wa barabara ya Malagarasi - Ilunde - Uvinza (km 51.1) kwa kiwango cha lami ukamilike ifikapo mwezi Machi, 2025.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo leo Julai 8, 2024 katika eneo la Malagarasi wakati akikagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Malagarasi - Ilunde - Uvinza kwa kiwango cha lami na kuridhishwa na maendeleo yake.
“Hii barabara imesuasua sana hasa kipindi cha mvua, na huku Kigoma bado tunapata mvua nyingi kwa hiyo Waziri tutumie kipindi hiki cha kiangazi kukimbiza hii barabara iishe kama ulivyoahidi na sisi tupite hapa tukiwa tumevaa suti, Simamieni hili Waziri pamoja timu yako”, ameeleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesema kuwa wananchi wa Kigoma wameisubiria barabara ya Uvinza - Malagarasi kwa muda mrefu na ni muda sasa ikamilike na wananchi waweze kuendelea kufanya biashara na kukuza uchumi wa Mkoa.
Amesisitiza kuwa uwepo wa miundombinu bora ya barabara kutaufanya Mkoa wa Kigoma kuwa Kitovu cha biashara na Mikoa mingine pamoja na nchi za jirani na kuwezesha wawekezaji kufika na kuwekeza katika Mkoa huo.
Dkt. Mpango ameagiza Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha hawapotezi ubora na viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa Mkataba.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa kipindi cha nyuma mradi wa ujenzi wa barabara ya Uvinza - Malagarasi ulikuwa una suasua hivyo Wizara ilichukua hatua ya kumuondoa Mhandisi Mshauri na kuleta Mhandisi Mshauri mwingine na sasa hivi ujenzi unaendelea vizuri.
Ameeleza kuwa baada ya hatua hiyo utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo hivi sasa unafanyika usiku na mchana na amemuahidi Makamu wa Rais kuisimamia barabara hiyo ikamilike kwa mujibu wa mkataba ifikapo mwezi Machi, 2025.
Bashungwa ameongeza kuwa hivi sasa kazi za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zinaendelea kuunganisha Mkoa wa Kigoma na Katavi ambapo wakandarasi wawili wamegawanywa katika barabara hiyo kwa vipande vya kilometa 25.
Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Uvinza - Malagarasi (km 51.1) umefikia asilimia 54 na sasa hivi kazi zinafanyika usiku na mchana ili mradi huo ukamilike kama ulivyopangwa.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Uvinza - Malagarasi unatekekelezwa na Mkandarasi kampuni ya STECOL Corporation na Mhandisi Mshauri Kampuni ya NORPLAN na unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 62.7.
Post A Comment: