Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameitaka Kampuni ya Nyati Minerals Sands inayotekeleza mradi wa uchimbaji Madini Tembo (Heavy Mineral Sands) katika Mikoa ya Dar es Salaam na Tanga kuanza uzalishaji mapema.
Aliyasema hayo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam, alipokutana na uongozi wa Kampuni ya Shenghe Resources Holding co. Ltd katika kikao kilicholenga kujadili maendeleo ya miradi hiyo. Kampuni ya Shenghe imepanga kununua hisa za asilimia 100 za Kampuni ya Strandline UK ambayo inamiliki hisa asilimia 84 za kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited.
Vilevile, Dkt. Kiruswa aliutaka uongozi wa kampuni ya Shenghe kuwasilisha Wizarani ratiba na mpango wa kampuni hiyo wa uendelezaji wa miradi hiyo na kuwataka kutekeleza miradi kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Madini.
‘’Sheria ya Madini Sura 123 inaelekeza wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini kuanza uzalishaji ndani ya miezi 18 baada ya kupewa leseni,’’ alisema Dkt. Kiruswa.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa aliupongeza uongozi wa kampuni ya Shenghe kuchagua kuwekeza Tanzania katika miradi mbalimbali na kusisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano ili kufanikisha uwekezaji wao.
Akiwasilisha mpango wa uendelezaji miradi, Mkurugenzi wa kampuni ya Shenghe Bi. Shasha Lu, alisema mpango kampuni ya Shenghe ni kuanza uzalishaji wa mradi wa Fungoni - Kigamboni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka 2024 na mradi wa tajiri Tanga, mwishoni mwa mwaka 2025.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Shenghe Bw. Huang Ping alimhakikishia Dkt. Kiruswa kuwa kampuni hiyo itaanza uzalishaji kama ilivyopangwa kwakuwa inauzoefu mkubwa wa kuendesha miradi ya madini mkakati na uwezo wa kifedha wa kuendeleza miradi hiyo ikiwemo ubobezi katika teknolojia.
‘’Tunaiomba Serikali ya Tanzania kutupatia ushirikiano ikiwa ni pamoja na kukamilisha kutoa vibali mbalimbali ili waweze kuwekeza nchini,’’ alisema Ping.
Aidha, uongozi huo ulionesha nia ya kuendeleza miradi mingine ikiwemo ya madini ya rare earth elements pamoja na viwanda vya uchakataji madini mkakati.
Post A Comment: