Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko ameagiza kujengwa kwa vituo vidogo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni ili kukabiliana na tatizo la umeme mdogo (Low voltage) na wakati mwingine kukatika mara kwa mara ilhali jitihada kubwa zimefanyika kumaliza tatizo la mgao nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo (Julai 7, 2024) wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ipole, Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora chenye KV 132.
“Kila anayeelewa hawezi kubisha kuhusu kazi kubwa iliyofanywa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uboreshaji wa huduma za jamii, hapendi na anachukizwa na mgao unaochelewesha huduma kwa wananchi”
Amesisitiza kujengwa kwa vituo vidogo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali kutadhibiti tatizo la nguvu ndogo ya umeme pale inapotokea hitilafu katika njia kuu ya umeme na pengine utadhaniwa kuwa ni umeme wa nishati ya jua ilhali ni umeme unotoka katika gridi ya taifa.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka watendaji wa TANESCO na kampuni zake Tanzu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati na kuelekeza apewe ripoti kuhusu hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa vituo hivyo ifikapo tarehe 15 Julai, 2024.
“Mwezi machi mwaka huu ujenzi ulikuwa chini sana lakini baada ya shinikizo na usimamizi ujenzi umepanda kwa kiwango kikubwa na hivyo kutatuwezesha kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwahiyo wapeni kazi wakandarasi na kuwasimamia tutapata matokeo” amesema Dkt. Biteko.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Gissima Nyamo - Hanga amesema ujenzi wa kituo cha Ipole utakamilika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu na kitou kitawahudumia wananchi wa Skonge, Kitunda na maeneo mengine ya Jirani.
Amesema hadi sasa kituo kimekamilika kwa silimia 97 na kitakuwa kikisambaza umeme kupitia msongo wa KV 33.
Kwa upande wake, Mbunge wa Sikonge, Mhe. Joseph Kakunda ameishukuru Serikali kwa hatua iliyochukuliwa kufikisha maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo na kumtaja Rais, Dkt. Samia kama kinara wa maendeleo nchini.
Post A Comment: