Na Denis Chambi, Tanga.
Mwenyekiti Chama cha Mapinduzi "CCM" Mkoa wa Tanga Mkoa wa Tanga Rajabu Abdulrahmani amekabidhi kiasi cha shilingi Milion 30 kama ada kwa ajili ya kuwawezesha madereva wa Daladala na Coaster zinazofanya safari zake ndani ya jiji la Tanga kupata mafunzo fani hiyo katika chuo cha ufundi stadi 'VETA' ili kukidhi vigezo vinavyotakiwa kutumia vyombo vya usafiri.
Madereva hao wapatao 600 watapata mafunzo kwa mwezi mmoja ndani ya chuo hicho cha ufundi stadi 'VETA' Tanga kikishirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani lengo likiwa ni kuwaongezea elimu na kuwawezesha kupata leseni ili kukidhi vigezo vya sheria za usalama barabarani ambapo wengine wao wamekuwa wakikamatwa na makosa mbalimbali yakiwemo ya ukosefu wa leseni za udereva.
Akikabidhi fedha hizo July 18,2024 katika ofisi ya Chama cha Mapinduzi mwenyekiti Rajabu Abdulrahmani amewaasa madereva kuendelea kuzingatia sheria za usalama barabarani huku akiwasisitiza kutojihusisha na vitendo vya rushwa pale wanapokamatwa mara baada ya kubainika kufanya makosa mbalimbali.
"Tukumbuke kuwa tukiendesha vyombo vya moto kiholela mnachangia kwa kiasi kikibwa sana kuhatarisha maisha yenu wenyewe madereva lakini pia na wale ambao mnawaendesha kwenye vyombo vya moto , ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inasimamia miongozo na sheria tuliyojiwekea kwa maslahi ya watanzania." amesema Abdulrahmani.
"Ni vibaya sana kumuona askari barabarani amekukamata na akakutoza faini kwa sababu ya uzembe wako mwenyewe halafu unakwenda kumuona ni mbaya lazima tupeane elimu na kuambiana sisi wenyewe kwa wenyewe, usifanye mapatano na askari pale unapokamatwa ukimkuta askari ambaye sio muadilifu, mpenda rushwa sasa ili yasitokee haya lazima tufuate utaratibu tutumie vyombo vya moto vikiwa vimetimia na kukidhi vigezo" alisisitiza.
Rajabu ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu Taifa na mjumbe wa kamati ya CCM Taifa ameongeza kwa kusema kuwa viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na Chama ngazi ya mkoa huo watahakikisha wanaendelea kuwainua wananchi wanaojishughulisha na shighuli za kujipatia kipato wakiwemo wajasiriamali wadogo wadogo ili kuwainua kiuchumi kwa hali na mali.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya kamanda wa kikosi cha usalama barabarani " RTO" Mkoa wa Tanga Inspekta Rajabu Ngumbi amekiri kuwepo kwa wimbi la madereva wengine ambao wamekuwa wakikamatwa kwa makosa mbalimbali ya kutokuwepo na leseni kama sheria za usalama barabarani zinavyotaka ambapo amesema kwa msaada huo walioupata madereva wengi wataweza kupata uhalali wa kuendelea na kazi zao.
Inspector Ngumbi amewaasa madereva kuchangamkia fursa hiyo ambayo itawasaidia kupata ajira kupitia makampuni na viwanda mbalimbali vilivyopo hapa nchini hususani katika jiji la Tanga.
"Hiki kilikiwa ni kilio chenu madereva cha muda mrefu sana viongozi wameshafanya yao sasa palipobakia ni nyie kutekeleza niwaombe sana msituangushe tumebahatika kuwa na viwanda vingi lakini tusijekuwa watazamaji mwekezaji anapokuja kuwekeza anategemea asilimia tisini ya madereva watoke ndani ya jiji la Tanga"Amesema Inspector Ngumbi.
Kwa upande wao mwenyekiti wa muungano wa wasafirishaji Abiria ndani ya jiji la Tanga 'MUWATA' Salim Jumbe pamoja na mwenyekiti wa chama cha 'TAREMIA' Ismail Masoud wamemshukuru na kumpongeza mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga kwa hatua hiyo aliyoifanya kuwashika mkono madereva ambao wengi wamekuwa wakishindwa kufanya shighuli hiyo kwa kukosa vigezo ikiwemo leseni za udereva.
Mkuu wa chuo cha ufundi stadi 'VETA' jiji la Tanga Gideoni Olelairumbe amesema kuwa kwa kuzingatia sheria na miongozo vya nchi juu ya ufundi stadi watahakikisha kwa kushirikiana na ofisi ya kamanda wa Polisi kikosi cha usalama barabarani pamoja na Mamlaka ya mapato Tanzania 'TRA' madereva wote wanamaliza masomo yao kwa viwango vinavyotakiwa.
"Hawa madereva tutakuwa nao pale VETA' kwa muda wa mwezi mmoja tutawagawa kwenye mkundi kulingana na mahitaji yao kwa sababu tunaamini wana mahitaji ya aina mbalimbali na ndio lengo letu la VETA hivyo nimewapokea vijana hawa tutatekeleza kama kanuni za nchi zinavyotaka kwa kushirikiana na ofisi ya TRO na TRA.
Post A Comment: