Wawakilishi 11 wa Bunge la Wawakilishi-Congress kutoka nchini Marekani wameridhishwa na juhudi za uhifadhi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania huku wakisifia namna ambavyo hifadhi za Taifa zimesheheni wanyamapori.
Hayo yamesemwa katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Wabunge hao kilichofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) leo Juni 1,2024.
Akizungumza kwa niaba ya Wawakilishi hao, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili kutoka Marekani ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arkansas, Mhe. Bruce Westernman amesema kuwa wamepata fursa ya kujifunza kuhusu uhifadhi na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
" Tumefurahi kujionea Wanyamapori wengi wakiwemo wanyamapori watano wakubwa ambao ni kivutio kikubwa cha utalii (big five) ambao ni Simba, Chui, Tembo ,Nyati na Kifaru" amesema.
Aidha, amesema katika kikao hicho wamepata fursa ya kujadiliana kuhusu kushirikiana hasa katika masuala ya uhifadhi, uwindaji wa kitalii na namna ya kuunga juhudi za pamoja katika kupambana na ujangili.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa amefurahi kukutana na ujumbe wa Kamati ya Maliasili kutoka Bunge la Wawakilishi la Congress.
“Tumewashukuru kwa namna ambavyo wameendelea kutoa ushirikiano na kusaidiana nasi kupitia Shirika la la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika jitihada mbalimbali za kuhakikisha tunakuwa na uhifadhi imara endelevu, harakati mbalimbali za kudhibiti ujangili pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusiana na suala zima la uhifadhi na kujua mipaka yao” Waziri Kairuki amesisitiza.
Vilevile, Mhe. Kairuki ametoa rai kwa Wabunge hao kuona namna bora ya kuendelea kushirikiana na taasisi zao hasa katika shughuli za uhifadhi na wanyamapori ili kuweza kuhakikisha kwamba uhifadhi wa Tanzania unaendelea kukua kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Wawakilishi wa Bunge la Wawakilishi-Congress kutoka nchini Marekani walianza ziara yao nchini Tanzania Mei 28,2024 na kuihitimisha Mei 31,2024. Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujifunza kuhusu Uhifadhi nchini Tanzania.
Post A Comment: