Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Arusha kuwekeza kwenye tafiti na utafutaji wa masoko ya bidhaa za kilimo zinazozalishwa na Wanachama wao.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Mtahengerwa ametoa kauli hiyo leo Juni 13, 2024 kwenye Viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Arusha, akihimiza kutumia vyema fursa ya mahitaji ya bidhaa za mbogamboga na nyama kutokana na wingi wa wageni wanaofika Mkoani Arusha.
Aidha Mkuu wa Wilaya Mhe. Mtahengerwa pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye Matumizi ya teknolojia za kisasa kwenye kilimo na ufugaji pamoja na kwenye vifungashio vya bidhaa za Kilimo na uchakataji wa vitoweo ili kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi mahitaji ya soko la Kimataifa.
Katika Hatua Nyingine Mhe Mkuu wa Wilaya akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa, amevitaka vyama vya ushirika Mkoani Arusha kuangalia upya viwango vya Riba za Mikopo wanayoitoa kwa wanachama wao, akitaka kuwa nafuu zaidi ili kutowaumiza wanachama wao na kusaidia kuwaondosha kwenye umaskini.
Post A Comment: