Kwa mafanikio makubwa, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limejitokeza kama moja ya taasisi za serikali zilizoshiriki katika utoaji wa gawio kwa mfuko wa Hazina ya Taifa zilizopokelewa na Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 11 Juni, 2024 Ikulu jijiji Dar es Salaam.
Gawio hilo limewasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Nah. Mussa Mandia pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nahson Sigalla.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi gawio hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bw. Nahson Sigala, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuchagiza Sekta ya Usafiri Majini na kupelekea matokeo ya ukusanyaji mzuri wa mapato.
"Tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi thabiti hasa katika sekta hii ya Uchukuzi na kusababisha na sisi TASAC Kuchangia katika mfuko huu wa Hazina ya Taifa kwa kiasi cha shilingi bilioni 19.057 kama matokeo mazuri ya utekelezaji wa majukumu yetu”.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alithibitisha kwamba TASAC imetoa gawio la shilingi bilioni 19.1 kwa mwaka unaoishia Juni 2024, huku akitoa shukrani za dhati kwa utendaji wao mzuri.
Hafla hizi zimefanyika katika ukumbi wa mikutano, Ikulu Ndogo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Wenyeviti wa Bodi, Wakurugenzi na Watendaji Wakuu na wa taasisi mbalimbali hapa nchini.
Aidha, Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan amesema hatakubali mtu yoyote amkwamishe kwenye azma yake ya kuleta mageuzi ya kiuchumi anayoendelea nayo na kwamba kila mmoja akafanye mageuzi ili kuongeza tija katika kukuza uchumi.
Amesema hataki kuona mtu yoyote anamkwamisha katika jambo hilo na kuwataka wakuu wa taasisi na viongozi wengine kuhakikisha wanaifanyia kazi falsafa hiyo na kuleta tija kwa Taifa na kuendelea kubakia katika uchumi wa kati.
"Hivi karibuni tumeingia tena kwenye kundi la uchumi wa kati kama ambavyo imeainishwa na wenzetu wa Benki ya Dunia, sasa ili uendelee kubakia katika kundi hilo ni lazima kuwe na mageuzi makubwa katika uchumi ili kuendelea kuaminika zaidi", amesema Rais Samia
Kuhusiana na mashirika yasiyofanya vizuri, Rais Samia amemtaka Msajili wa Hazina kuhakikisha anasimamia zoezi hilo na akishindwa basi yeye mwenyewe (Rais Samia) ataingilia kati na kuyafuta.
Amerudia tena agizo lake la kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana ifikapo mwezi Disemba mwaka huu bila kuwa na kisingizio chochote.
Post A Comment: