Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema Tanzania tuitakayo Mwaka 2050 ni ile ambayo Watanzania watakuwa vinara kuiongoza sekta ya madini na kunufaika na sekta ya madini na hivyo kupelekea sekta ya madini kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu ya Tanzania.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 08 Juni, 2024 katika Ukumbi wa Nkurumah Chuo Kikuu cha Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Kitaifa kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 lililofunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango.
Akizungumza kwenye kongamano hilo,Mh Mavunde ameeleza kupitia Sekta ya Madini Tanzania tuitakayo 2050 tunataraji iwe na Sifa kadha wa kadha ikiwemo kuwepo na taarifa za miamba ambazo zitasaidia kuwaondoa watanzania kwenye uchimbaji wa kubahatisha kupitia utekelezaji wa VISION 2030 yenye lengo la kufanya utafiti wa kina wa uwepo wa madini.
Aliongeza kuwa, anataraji kuiona Tanzania ambayo inaongeza thamani madini hapa nchini hususan madini mkakati ambayo ndiyo mwelekeo wa dunia kwa sasa, anatamani kuona betri za magari ya umeme zikitengenezwa hapa nchini na kwenda kufungwa moja kwa moja kwenye magari ya umeme kokote duniani yanakotengenezwa.
Pia, kupitia usimamizi thabiti na weledi wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tunataraji kuiona Tanzania yenye uchumi mkubwa ulioshikiliwa na wazawa baada ya kuwezeshwa kupitia Local content ili washiriki kikamilifu katika uchumi wa Madini hususan katika utoaji wa huduma.
Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kwamba ni matarajio ya Wizara kuhakikisha inaliwezesha Shirika La Madini Tanzania kuwa Shirika Kiongozi kupitia umiliki wa Migodi mikubwa na ya kimkakati ili kuongeza manufaa kwa Taifa kupitia rasilimali madini ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia.
Vilevile, Mavunde alianisha sifa nyingine kuwa ifikapo 2050 ni kuongezeka kwa Mchango wa Wachimbaji wadogo kwenye ukuaji wa sekta na Pato la Taifa, kutokana na kuwezeshwa mitaji na maeneo ya uchimbaji yaliyofanyiwa utafiti.
Akihitimisha, Waziri Mavunde alitanabaisha kuwa anaiona Tanzania 2050 ambayo itakuwa ni Kitovu cha utoaji wa Huduma na usambazaji wa bidhaa za migodini kutokana na uanzishwaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodi nchini, tofauti na hali ya sasa ambapo bidhaa nyingi za migodini zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Post A Comment: