Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameieleza jumuiya ya wafanyabiashara wa ujerumani na wadau wa nishati kuwa Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele kwenye vyanzo mbadala vya nishati ikiwemo gesi, upepo, jua na vyanzo vingine mbadala vya umeme, ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme wa kutosha kwa wananchi.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Juni 11, 2024 alipokutana na ujumbe wa chemba ya wafanyabiashara na wadau wa sekta ya nishati kutoka Ujerumani wakiongozwa na Balozi wa shirikisho la ujerumani nchini Mhe. Thomas Terstegen.
‘’Nipende kuwashukuru wenzetu wa Ujerumani kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwenye sekta ya nishati hususani kwenye miradi ya umeme ambapo wamekuwa wakifadhili na kutoa mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo’’ Alisema Dkt. Biteko.
Alisema Nishati inabeba ajenda kubwa nchini Tanzania ikiwemo usalama wa nishati yenyewe, upatikanaji wa nishati na uhakika wa nishati kama ilivyoainishwa kwenye sera ya nishati ya mwaka 2015 na kuongeza kuwa serikali imejipanga kufikisha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2030
Alisema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wadau na makampuni mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya uwekezaji yanapewa fursa ili kutekeleza miradi iliyoainishwa na imekosa fedha ili kutumia fursa hiyo kuwekeza kwa pamoja na wadau wa sekta binafsi.
Akitoa tathmini ya hali ya upatikanaji wa umeme Dkt. Biteko alisema kwa sasa ongezeko la mahitaji ya umeme kwa Tanzania yanakuwa kwa asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka kutokana na kuongeza kwa mahitaji, wateja na shughuli za kiuchumi na kuongeza kuwa vyanzo vya umeme vinavyotegemewa ni maji ambapo inachangia asilimia 39, gesi asılıa inachangia asilimia 56.1 mafuta asilimia 4.3 na vyanzo vingine 0.5
Kwa upande wake, Balozi wa Shirikisho la Ujerumani Mhe.Thomas Terstegen alisema Tanzania imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na nchi ya ujerumani hususani kwenye sekta ya nishati na kuahidi kuendelea kufadhili na utekelezaji wa miradi kwenye sekta ya nishati ili kuinua uchumi wake.
Aidha, mkutano huo ulilenga pia kutoa fursa kwa wadau wa sekta binafsi na nishati kufahamu fursa zilizoko nchini ujerumani na namna ya kuzitumia na ambao ulihudhuriwa na Maren Diale Schellschmidt ambae ni Mkuu wa Msafara kutoka chemba ya wafanyabiashara na Viwanda kutoka Afrika, wawakilishi kutoka shirikisho la watu wa Ujerumani, wawakilishi kutoka Serikalini na kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wa sekta ya nishati.
Post A Comment: