Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Serikali imefanikisha kupatikana kwa maeneo 15 ambayo yatatolewa leseni 15 kupitia Umoja wa Wanawake Wachimba Madini Mkoa wa Geita (GEWOMA) baada ya umoja huo kukamilisha usajili.
Ameyasema hayo, leo Juni 04, 2024 Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Sylvia Sigula aliyetaka kujua Serikali imetoa motisha kiasi gani kwa Wanawake 300 walioahidiwa kununuliwa Leseni za Uchimbaji Madini na Mheshimiwa Rais.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Leseni hizo zitakapotolewa vitaundwa vikundi vya wanawake 20 katika kila eneo ambapo ni sawa na idadi ya wanawake 300 kwa leseni zote, na kwamba Leseni hizo zitalipiwa ada zote muhimu na Serikali kwa kipindi cha awali.
Aidha, amesema kuwa Serikali imeanzisha programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) ambayo inalenga kuboresha Sekta ya Madini kwa kuweka mazingira bora zaidi ya kuwezesha uchimbaji kwa wanawake na vijana.
Ameongeza kuwa, Mpango huo wa MBT unajumuisha mafunzo kwa wachimbaji, kuboresha teknolojia za uchimbaji, na kuhakikisha uchimbaji unafanyika kwa njia endelevu na yenye tija.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imefanya jitahada mbalimbali kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini ya chumvi katika Wilaya ya Manyoni, hususani katika kutoa mafunzo ya uchimbaji wa Madini ya Chumvi pamoja na uchakataji wake kwa kutumia nishati mbadala ya makaa ya mawe badala ya utumiaji wa kuni wanaoutumia kwa sasa.
Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Mhe. Dkt. Pius Chaya aaliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwekeza kwenye Madini ya Chumvi na Magadi katika Kata za Majiri na Sanza Wilaya ya Manyoni.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, takribani wachimbaji wadogo 60 wa kikundi cha wachimbaji wa chumvi katika Kijiji cha Kinangali Wilayani Manyoni walipata Elimu hiyo.
Ameongeza kuwa, Vilevile, Serikali kupitia STAMICO inaendelea na mpango wa ujenzi wa Kituo cha mfano cha uchakataji chumvi katika Mkoa wa Lindi ambako Kiwanda hicho kitatumika kuchakata chumvi na kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wazalishaji wa chumvi ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha kwa tija na ubora stahiki wakiwemo wazalishaji wa Chumvi Manyoni mkoani Singida.
Post A Comment: