Na Denis Chambi, Tanga.
MKUU wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani ameiagiza halmashauri ya Handeni vijijini kuhakikisha inatenga fedha ili kuweza kulipa madeni ya Shilingi Bilioni 2.306 inayodaiwa na watumishi pamoja na wazabuni jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali.
Dkt Buriani ametoa maelekezo hayo Juni 21,2024 wakati akiwa kwenye kikao cha Baraza maalum la kupokea taarifa za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo halmashauri hiyo ilipata hati inayoridhisha ikiwa ni mwaka wa tano mfululizo.
"Pamoja na hati safi tuliyoipata na pamoja na kujibu hoja kuna mambo ambayo yametusababishia halmashauri yetu kuwa na hoja hizi nyingi ambayo yako ndani ya uwezo wetu na tukikubaliana kwa pamoja tunaweza kuyapunguza"
" Kwa mfano madeni ya watumishi Handeni ni halmashauri pekee kushinda halmashauri zote yenye madeni mengi ya watumishi na wazabuni lakini pia hata ule utayari wa kulipa hauonekani na fedha mnayotenga kulipa, mna madeni ya Bilion 2.306 na fedha mnayotenga ni Milion 24 hii tunaona kama ni takrima , tunaelekeza mtenge fedha za kulipa madeni ya watumishi na wazabuni haipendezi hawa watu wanakwenda mpaka kwa waziri Mkuu kudai madeni jambo hili mkalisimamie" alisisitiza Dkt Buriani.
Sambamba na hilo mkuu huyo wa mkoa ameitaka halmashauri kulipa deni la kiasi cha shilingi Million 17 ambalo linadaiwa na watumishi wastaafu katika halmashauri hiyo ambapo ameelekeza kabla ya kufika Juni 30 deni hilo liwe limeshalipwa.
"Watumishi wastaafu wanadai shilingi Million 17 hili ni Deni la kufuta kabisa tuhakikishe kabla ya kufika Juni 30, 2024 hili deni la watumishi wastaafu liwe limefutwa kuna mambo mengine ambayo ni lazima tuyasimamie na kuuatekeleza wenyewe" alisema.
Aidha Dkt Buriani amemwelekeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuandaa na kufanya tathmini ya miradi yote viporo ambayo imeshindwa kumalizia kwa wakati ikiwemo ya tangu 2008 ambapo yote kwa pamoja inaghalimu zaidi ya shilingi Milion 600 akitaka kuelezwa ni hatua gani zimechukuliwa ili kuikamilisha.
"Vile vile miradi kutokukamilika imechochea hoja za 'CAG' na mapungufu mbalimbali yaliyoonekana katika miradi ambayo ina thamani ya shilingi million 600 kuna miradi ya toka mwaka 2008 na 2009 na ni kama hatujui tunaenda wapi , mkurugenzi fanya tathmini miradi yote iliyopo na hatua iliyofikia na tujue ni namna gani mmejipanga kuweza kuikamilisha ni jukumu letu kufuta hizi hoja "
Awali akitoa taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali Hamu Mwakasola ambaye ni mkaguzi wa nje wa mkoa wa Tanga amesema katika mapendekezo 41 sawa na asilimia 71 yametekelezwa mengine 17 yakiwa bado akiitaka halmashauri hiyo kuendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa.
"Kwa hesabu za mwaka wa fedha 2022/2023 hali ya utekelezaji wa hoja za mkaguzi inaonyesha kwamba mapendekezo 41 sawa na asilimia 71 yametekelezwa mengine 17 bado yamebaki naomba nitoe rai kwa viongozi na watendaji kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji"
Akipokea maelekezo hayo kutoka kwa Mkuu wa mkoa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Handeni vijijini Saitoti Zerote amesema kuwa watahakikisha yale yote ambayo yaliibuliwa kwenye taarifa ya hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wanakwenda kuyatekeleza kwa vitendo.
Alisema kuwa halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ilipangiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilion 2, 561 huku wakiongezewa kiwango cha shilingi Milion 450 ambapo mpaka sasa imefikisha makusanyo ya asilimia 120.
"Tumepokea maelekezo ya mkuu wa mkoa na tutakwenda kuyatekeleza kwa vitendo na kwa wakati , kwa mwaka huu wa fedha halmashauri yetu ilipangiwa kukusanya shilingi Bilion 2,561 lakini katibu tawala wa mkoa alituridhia na kukuongezea shilingi milioni 450 katika bajeti yetu sasa hivi tuna asilimia 120 mpaka June 30,2024 nina imani kabisa tutafika asilimia 125" alisema Zerote.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza la madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mussa Mwanyumbu alisema mpaka kufika December 2024 hoja zote ambazo zilitolewa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali zitakuwa zimefutwa.
"Tutahakikisha na tumekubaliana na kamati yetu ya fedha kwamba mpaka ifikapo December 2024 hoja zote zioizobaki zitakuwa zimefutwa hayo ndiyo maoni ya Baraza letu mkuu wa mkoa tunakuhakikishi hilo"
Post A Comment: