Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka amesema ametaka kuwatafuta Wahudumu wa Afya wazuri ambao watakwenda kufanya kazi hiyo kwa ueledi.

 Rc Mtaka amebainisha hayo Mkoani Njombe katika Semina elekezi kwa viongozi na Wataalam ngazi ya Wilaya na Mkoa wakati wa Mchakato wa kuwapata Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.

 "Mhe. Rais anafanya mageuzi makubwa sana kwenye sekta ya Afya ,niwaombeni watu mnaosimamia zoezi hili zingatieni kuweka watu wenye sifa,wekeni matangazo waelimisheni wapate watu wenye sifa wakibeba haiba njema ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Mfamasia kutoka Wizara ya Afya Oscar Kapera amesema miongoni mwa sifa ya Wahudumu hao ni elimu kuanzia Kidato cha nne. 

"CHW ambaye atachaguliwa atatakiwa angalau awe amemaliza Kidato cha nne, sifa nyingine awe mkazi wa eneo husika na awe anafahamu utamaduni, mila na desturi za jamii husika, awe amekubalika kimaadili na Kiutamaduni ,lakini pia awe na kitambulisho kinachotambulika rasmi mfano NIDA,leseni na vitambulisho vingine ambavyo vinatakiwa,asiwe na historia ya vitendo vya kihalifu mfano unyanyasaji wa kijinsia ,ukatili kwa watoto,awe na moyo wa kujituma, mchapakazi na awe mwaminifu wa kutunza siri ,awe na umri usiopungua miaka 18 na isiyozidi miaka 55"amesema. 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mpanga amesema awali mkoa wa Njombe utaanza na Halmashauri mbili za Njombe Mji na Njombe Vijijini ikiwa ni mkataba wa miaka mitano utakaokwenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa Wahudumu hao. 

"Mwanzoni Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii walionekana kama wanatumika kila mmoja anatumia kivyake,lakini sasa hivi kutakuwa na Mpango Maalum Jumuishi watafanyiwa Mafunzo kwa miezi 6 kuna Programu zimeandaliwa watakazofundishwa,kila kijiji au mtaa kutakuwa na wawakilishi wawili"amesema.

 Ikumbukwe kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza Programu Maalum ya kuwatambua Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii(CHW) kwa kuwapa Mafunzo na ajira ndogondogo ili kupunguza changamoto kwa wananchi katika Sekta hiyo.

Share To:

Post A Comment: