Akimkaribisha Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi Mkoani Arusha leo Juni 2, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameapa kuendelea kuwawajibisha watumishi na watendaji wazembe na wabadhirifu ili kuhakikisha malengo na ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatekelezwa kikamilifu.
Mhe. Makonda amesema hayo wakati akiwa wilayani Monduli eneo la Makuyuni na kumuahidi Katibu Mkuu wa CCM kuwa atasimamia maelekezo na maagizo yote ya Chama Cha Mapinduzi katika kutimiza maono na matamanio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Katika kuwatumia wananchi.
Mhe. Makonda pia amemueleza Katibu Mkuu wa CCM kuwa Mkoa wa Arusha unaendelea kufanya vyema kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii ambayo ameelekeza nguvu zake huko katika kuikuza na kuipa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa anatekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wa Arusha.
"Mhe. Nchimbi karibu kwenye Mkoa wa wajanja kuliko mikoa yote duniani, watu wakweli, majasiri na wasioyumba kusimamia haki zao, Mkoa ambao unaongoza kuunganisha si tu kwa Tanzania bali bara zima la Afrika katika utalii. Mkoa wenye wafugaji na wanaojua thamani ya mifugo, Mkoa wa wachimbaji wanaotangaza duniani umuhimu wa Tanzanite." amesema Mhe. Makonda.
Katika hatua nyingine Mhe. Makonda ameitaja changamoto kubwa inayousumbua mkoa wa Arusha kuwa ni migogoro ya ardhi na amekiahidi Chama Cha Mapinduzi CCM kuwa atahakikisha anamaliza migogoro yote ya ardhi katika kipindi chake cha Uongozi akishirikiana na Waziri wa ardhi.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Balozi Nchimbi pamoja na wajumbe wengine wa Kamati kuu ya CCM wapo Mkoani Arusha kwa ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM pamoja na kutatua kero za wananchi ambapo Jumatatu ya Juni 3, 2024 wamepangiwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya kituo cha mabasi cha Kilombero Jijini hapa.
Post A Comment: