Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameonesha kufurahishwa na mikakati iliyowekwa na Mkoa wa Kimadini Shinyanga ya ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali ambayo hadi kufikia Juni 17, 2024 kiasi cha shilingi bilioni 24.3 kimekusanywa sawa na asilimia 97.4 ya lengo la makusanyo ya mwaka.
Baadhi ya mikakati iliyobainishwa ni pamoja na kuendelea kufungua zaidi vituo vya ukaguzi wa madini ujenzi hususan Wilaya ya Kishapu na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambako imebainika uwepo wa shughuli nyingi zinazotumia madini ya ujenzi.
Hayo yamebainishwa leo Juni 19, 2024 ambapo Mbibo ameendelea na ziara yake ya kikazi kutembelea na kukagua shughuli za madini zinazofanywa katika mikoa mbalimbali ikiwemo kuzungumza na watumishi ili kusikiliza kero na changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kujionea maendeleo ya shughuli za madini.
Mikakati mingine iliyotajwa ni pamoja na kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi mbalimbali za fedha zikiwemo benki ili kuweza kuwakopesha wachimbaji wapate zana za kisasa pamoja na kuendelea kusimamia wachimbaji pale wanapopata wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye uwezo kiuchumi na wenye nia ya kuwapa msaada wa kiufundi (Technical support).
Vilevile, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi kwa kushirikiana na ofisi ya Meneja wa TANESCO Shinyanga, wameweka mkakati wa kufuatilia kwa ukaribu na kuhakikisha mchakato wa kupelekwa kwa umeme kwenye maeneo ya uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu ili kusaidia kuanza kutumika kwa mitambo ya kisasa yenye tija.
Mbali ya kutembelea shughuli za madini, pia, Mbibo amefanya kikao na watumishi wa ofisi hiyo ambapo amewataka kuweka mkazo katika shughuli za ukaguzi wa migodi, kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji kuhusu masuala ya usalama, utunzaji mazingira ili kuepusha ajali na uharibifu wa mazingira.
Katika hatua nyingine, Mbibo amefanya kikao na timu ya wakaguzi wa migodi kutoka Tume ya Madini Makao Makuu ambayo ipo mkoani humo kwa shughuli za ukaguzi.
Mkoa wa Kimadini Shinyanga una soko kuu moja la biashara ya madini pamoja na vituo vitano vya ununuzi wa madini ya almasi na dhahabu.
Post A Comment: