MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, ameanzisha mfumo maalum wa kidigitali wa kuwasilisha kero za wananchi kupitia wenyeviti wa mitaa ambao utawezesha changamoto na kero za wananchi kufanyiwa kazi kwa uharaka kupitia ofisi ya Mbunge.


Mbunge Mavunde ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wenyeviti wa mitaa 222 wa Jiji la Dodoma katika mkutano maalum ulioandaliwa na uongozi wa CCM wilaya ya Dodoma Mjini kujadiliana namna bora ya kutatua changamoto za wananchi katika ngazi za mitaa.


“Kwanza tunaishukuru sana serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushughulikia kero nyingi za kimsingi zinazowahusu wananchi wa Dodoma.


Kupitia ofisi yangu ya Mbunge, tutaweka mfumo maalum wa mawasiliano baina ya Mbunge na Wenyeviti wa mitaa ili kushughulikia kero za wananchi kwa wakati na mfumo huu unatengenezwa na Vijana wanufaika wa mkopo wa 10% wa Jiji la Dodoma wajulikanao kama 'Dodoma Tech Company Ltd'.


Pia mfumo huo,kwa kushirikiana na Kampuni ya Raddy Electronics ya Mkuranga,Pwani tutagawa simu janja kwa wenyeviti wote ambazo zitaungwa moja kwa moja kwenye mfumo.


"Lengo letu hapa ni kurahisisha mawasiliano kati ya Viongozi wa Mitaa,Diwani na Mbunge katika kutatua changamoto na kero za wananchi ”Alisema Mavunde


Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya Cde Charles Mamba, amewataka viongozi wote wachaguliwa wa wananchi wanakuwa wa kwanza kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao badala ya kuwaacha wananchi kutembea katika ofisi mbalimbali kutafuta msaada ilihali wenyewe wapo na kusisitiza chama hakitasita kumchukulia hatua mchaguliwa yoyote ambaye hatatimiza majukumu yake ya msingi.


Akishukuru kwa niaba,Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa wote wa Dodoma Jiji ,David Ndejembi, amemshukuru Mbunge Mavunde kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa uongozi wa mitaa katika kutatua changamoto za wananchi na kutumia fursa hiyo kumshukuru kwa mchango wa upatikanaji wa ofisi na ununuzi wa samani kwa ajili ya ofisi ya umoja huo.

Share To:

Post A Comment: