Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini unaonesha maendeleo mazuri na umeendelea kuimarika kutokana na juhudi za serikali sambamba na mwitikio mkubwa wa wananchi pamoja na wadau.
Hayo yameelezwa leo Juni 5, 2024 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Tamima Haji Abass (CCM) ambaye alitaka kujua mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini.
Waziri Ummy amesema mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini unaonesha maendeleo mazuri na umeendelea kuimarika kutokana na juhudi za Serikali sambamba na mwitikio mkubwa wa wananchi pamoja na wadau.
Waziri Ummy amesema Serikali imepanua wigo wa uelimishaji na uhamasishaji wa masuala ya lishe kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo Vyombo vya Habari ikiwemo Redio, televisheni, na mitandao ya kijamii kote nchini na katika mikusanyiko ya kijamii hususani wakati wa maadhimisho mbalimbali.
Amesema pia uwepo wa mtaala wa Elimu ambao umejumuisha masuala ya Afya na Lishe kwa ngazi ya Msingi na Sekondari unaotoa fursa kwa wanafunzi kujifunza.
Amesema ili kupata uelewa wa elimu ya lishe Wizara imezindua mwongozo wa Kitaifa wa chakula na ulaji mwezi Novemba 2023 wenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya chakula mchanganyiko kwa kuzingatia vyakula vinavyopatikana hapa nchini.
Waziri Ummy amesema Elimu ya lishe imeendelea kutolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini hususani wakati wa Kliniki za mama na mtoto na kliniki za wagonjwa wengine wa nje.
Pia uhamasishaji kupitia Ujumbe wa mbio za Mwenge mwaka 2024 ambao una kauli isemayo “Lishe sio kujaza Tumbo, Zingatia unachokula".
Post A Comment: