Kituo cha Uwezeshaji Wananchi kiuchumi kilichopo chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kimezinduliwa Wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Akiongea na wananchi wa Nyang’hwale mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Sabasaba, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’ Issa alisema kuwa huduma zitakazo patikana katika kituo hicho ni pamoja na Urasimishaji wa Biashara, Ushauri wa Biashara, Elimu na mafunzo ya Ujasiriamali.
Aliongeza kuwa, kituo hicho kitarahisisha huduma ya upatikananji wa mitaji nafuu, upatikanaji wa taarifa za masoko, Upatikanaji wa Teknolojia na ufundi, Elimu ya vikundi vya kifedha na kijamii ikiwemo vyama vya ushirika vya akiba na mikopo na uongezaji wa thamani za bidhaa.
“Lengo la kuanzishwa kwa vituo hiki ni pamoja ya kuwaondolea adha wakulima na wafanyabiashara wenye lengo la kupata huduma na masoko na kurasimisha biashara zao, vilevile kupata Elimu kwa haraka ndani ya jengo moja kutoka kwa Taasisi mbalimbali zitazokuwa zikifanya kazi katika Kituo hicho,”Alisema Katibu Mtendaji huyo.
Aliendelea kwa kuzitaja baadhi ya Taasisi zitakazokuwepo katika Jengo hilo akiwa ni pamoja na shirika la viwanda vidogo SIDO, Mfuko wa pembejeo za kilimo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara (BRELA) Wakala wa Usalama Kazini (OSHA) Mabenki pamoja na kampuni mbalimbali za Uendeshaji Biashara.
“Mhe. Waziri Mkuu Tumekuwa na mafanikio makubwa sana katika vituo hivi hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo na huduma kwa wateja, na kutoa huduma mbali mbali za kibiashara kwa wafanyabiashara,” Alifafanua Bi.Beng’ Issa
Kituo cha Uwezeshaji wananchi Kiuchumi kilichozinduliwa Nyang’hwale ni Miongozi mwa vituo kadhaa vilivyopo hapa nchini ambacho kinatarajiwa kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya.
Kwa Upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha katika Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambayo imewawezesha kutekeleza programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu tutaendelea kulisimamia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ili liweze kufanya vizuri katika uwezeshaji wananchi kiuchumi,”Alipongeza Mhe. Nderiananga.
Post A Comment: