Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Paul Christian Makonda amesema maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 yanayotarajiwa kuanza Juni 7 Mwaka huu yatachochea na kusisimua Utalii wa Arusha kwa kiasi kikubwa, akiwataka wananchi na Wadau wa Utalii kuchangamkia fursa ya uwepo wa maonesho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 5, 2024 mara baada ya kukagua maandalizi ya maonesho hayo yatakayofanyika kwenye viwanja vya Magereza Arusha na kufunguliwa na Waziri wa Maliasili na utalii Mheshimiwa Angellah Kairuki.
Maonesho hayo yanatarajiwa kushirikisha Makampuni ya Kimataifa zaidi ya 700 kutoka kwenye Mataifa takribani 50 na yakitarajia kushirikisha Makampuni wenyeji zaidi ya 500 yatakayoonesha bidhaa na kazi mbalimbali kwenye maonesho hayo.
Mhe. Paul Christian Makonda amewataka wadau wa utalii kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ili kutangaza huduma zao pamoja na kubadilishana uzoefu na makampuni mengine ili kuweza kusaidia kukuza utalii Mkoani Arusha.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha kadhalika amewakaribisha wananchi na Raia wote wa kigeni kwenye maonesho hayo akiwahakikishia suala la Ulinzi na usalama kwa muda wote wa maonesho hayo yatakayofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Juni 07 mwaka huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Kili Fair Bwana Dominic Shoo amemuambia Mkuu wa Mkoa kuwa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 95 akisisitiza kuwa maonesho ya mwaka huu yameboreshwa zaidi ikiwemo kuongeza saa za maonesho hayo pamoja na kutenga maeneo maalum kwaajili ya michezo ya watoto.
Maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 yanafanyika kwa awamu ya tisa Jijini Arusha likiwa ni jukwaa maalum la kuyaweka pamoja makampuni ya ndani na nje ya nchi yanayohusika na sekta ya Utalii ili kuwakutanisha pamoja na kubadilishana bidhaa, huduma na uzoefu unaotokana na sekta ya Utalii duniani.
Post A Comment: