Na Jenipher Jamal – REA
Bodi ya Nishati Vijijini (REB) ikiambatana na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametembelea kiwanda cha kutengeneza vifaa vya umeme cha Elsewedy Electric kilichopo Dar es Salaam na kuridhishwa na uwepo wa vifaa vya kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini.
Ziara hiyo imefanyika Juni 13 mwaka huu, kwa lengo la kujionea uwezo wa viwanda vya ndani vinavyotengeneza vifaa vya umeme, ambavyo kwa kiasi kikubwa ndivyo hutumika katika miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na REA.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi, Mhe. Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) Jacob Kingu amesema kuwa miradi ya kupeleka umeme vijijini imechochea uwepo wa wawekezaji katika uzalishaji wa vifaa vya kusambaza umeme.
“Tumetembelea kiwanda hiki ili kujionea uwezo wao wa kuzalisha malighafi tunazotumia katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kusambaza umeme vijijini kama vile waya pamoja na mashime umba (tranfoma) pamoja na vifaa vingine vinavyotumika katika usambazaji wa umeme vijijini.
Tumejiridhisha kuwa kiwanda kina uwezo mkubwa. Aidha, ni jambo zuri kuwa uwepo wa REA umekuwa ni kichocheo kikubwa cha kampuni kama hizi kuja kuwekeza hapa nchini hivyo kuwezesha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vinavyohitajika katika miradi ya umeme badala ya kuagiza kutoka nje,” amesema Mwenyekiti.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa kwa sasa REA inatekeleza miradi mingi ya kupeleka umeme vijijini na kwamba uwepo wa kampuni kama hizo umewezesha miradi kutekelezwa kwa wakati, akifafanua kuwa hali ingekuwa tofauti endapo Serikali ingelazimika kuagiza vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
“Kwa sasa tuna mikataba takribani 137 inayoendelea ambayo yote inahitaji vifaa vya umeme na wakandarasi wengi wananunua vifaa kutoka hapa. Pia, tuna mradi mkubwa sana wa kupeleka umeme katika vitongoji 32,000 na sasa ni wakati muafaka kujiridhisha endapo miradi hii itapata vifaa vyote kutoka nchini. Tumejiridhisha kuwa Elsewedy wana uwezo na wanazalisha vifaa vya kutosha. Hivyo, vifaa kutoka kwao tukiunganisha pamoja na vinavyozalishwa na viwanda vingine nchini, tunaamini miradi yetu itakwenda vizuri,” amesema Mhanisi Olotu.
Olotu amesema kuwa Sera ya REA ni kuwapa kipaumbele wazalishaji wa ndani ili kuchochea ajira kwa vijana wa Kitanzania lakini pia urahisi wa kupata vifaa hivyo kwa wakati tofauti na ukiagiza kutoka nje.
Awali, akizungumza kuhusu kiwanda hicho, Mwakilishi wa Uongozi wa kiwanda hicho, Gloria George amesema kuwa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha Tani 15,000 pamoja na mashine umba 2,500 kwa mwaka na kuongeza kuwa REA ni miongoni mwa wateja wao wakubwa.
“Asilimia 90 ya vifaa vyetu tunavyozalisha hapa vinaenda kwenye miradi ya umeme inayotekelezwa na REA pamoja na TANESCO. Tunawashukuru sana kwa kuendelea kutushika mkono kwa kununua kwetu vifaa mbalimbali na kwa kufanya hivyo imekuwa ni chachu ya kukuza ajira kwa vijana wa Kitanzania kufanya kazi hapa,” amesema Gloria.
Post A Comment: