Na Denis Chambi, Tanga.


WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu ametoa onyo kwa baadhi ya wahudumu wa afya wanaouza dawa za Amoxicillin DT kwa watoto wenye umri chini ya  miaka mitano wakati wanapoenda kupatiwa matibabu  ambapo dawa hizo kwa maelekezo ya Serikali hutolewa bure.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo mkoani Tanga wakati akikabidhi gari ya kubebea wagonjwa 'Ambulance' katika kituo cha afya Duga  kilichopo Jiji la Tanga  ambapo amebainisha kuwa gari hilo ni miongoni mwa Magari zaidi ya 600 yanayosambazwa nchi zima na wizara ya afya kwa kushirikiana na ofisi ya Rais tawala za mikoa na Serikali za mitaa 'TAMISEMI'  lengo likiwa ni kutokomeza vifo vya wagonjwa wakiwemo wajawazito wanapohitaji huduma za dharura.

"Lengo letu ni kuboresha huduma za rufaa kwa wagonjwa  tunataka tusipoteze watu kwa sababu  wagonjwa walikuwa wanafariki kwa sababu ya kukosa huduma kwa wakati hususani wagonjwa wa dharura"

Akizungumzia changamoto ya dawa zinazouzwa  kinyume na maelekezo ya Serikali , Waziri Ummy amewataka wahudumu wa afya  kuzingatia sera ya afya bure kwa wamama wajawazito na watoto.

"Kama dawa zipo hamna haja ya kumwambia mgonjwa changia  zingatieni sera ya matibabu kwa wamama wajawazito na watoto waliopo chini ya miaka mitano , nimeangalia daftari la wagonjwa kati ya 10  watoto waliokuja hospital  7 wana maambukizi ya Bakteria ambayo inatibiwa na dawa inaitwa Amoxicillini DT.

"Dawa hii ya a Amoxicillin DT  haipaswi kuuzwa kwa watoto waliopo chini ya miaka mitano na hili nalisisitiza tuzingatie maelekezo ya Serikali  , kwa sababu tumeona inauzwa mwaka huu tutaandika haiuzwi sasa ole wake tuikute kwenye Duka inauzwa utatuambia umeitoa wapi"

Katika kulidhibiti hilo waziri Ummy amesema watatoa semina elekezi kwa viongozi kuanzia ngazi za vijiji na vitongoji ili kutokomeza tabia hiyo ya baadhi ya watoa huduma ikiwemo maduka ya dawa  kuuza dawa ambazo Serikali imeelekeza zitolewa bure kwa wagonjwa.

"Itabidi tuende mpaka ndani tuweke alama utakapoonoa hii dawa imeandikwa GOT ukiiona jua kuwa imeibiwa na haipaswi kuuzwa hizi dawa zinanunuliwa na Serikali na kusambaza hii ndio sera ya matibabu bure, tutafanya semina kwa viongozi wa Serikali  kuanzia ngazi za mtaa  kuhusu hili" alisema Ummy..

Aidha Waziri Ummy amepiga marufuku wamama wajawazito kuuziwa  kadi za Kliniki mara tu wanapofika katika vituo vya afya ambapo amesema haziuzwi huku akieleza kuwa wizara imekuja na mfumo mpya wa kadi ambazo zitarahisisha kupata taarifa za mjamzito tangu awali.

"Ni marufuku kuwauzia wamama wajawazito kadi za Kliniki wizara ya afya tumesambaza kadi ni aibu kumuuzia mama mjamzito kadi ya Kliniki na kama kadi hizo hakuna nyie wenyewe madaktari mkachapishe , na  sasa hivi tumetoa kadi mpya ambazo zipo kama kitabu ambacho kitakuwa ni rahisi kufuatilia taarifa za mjamzito Kuna mambo mengine tusiichonganishe Serikali na wananchi"alisisitiza.

Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa gari hilo la wagonjwa wananchi  wameishukuru na kuipongeza Serikali kuwaondolea adha hiyo ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo hususani muda wa usiku.

Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Neema Charles amesema awali walikuwa wakitoka rufaa kwa wagonjwa kupitia Ambulance vituo vingine hali ambayo imekuwa ikichelewesha huduma pale inapotokea mgonjwa wa dharura lakini kutokana na ujio wa ambulance waliyokabidhiwa  itakwenda kuondoa kero hiyo.

"Ambulance hii inakwenda kuondoa kero iliyokuwepo kituoni hapa tulikuwa tukitoa rufaa kwa wagonjwa lakini tunatumia Magari kutoka vituo vingine  kwahiyo wagonjwa walikuwa wanachelewa kufuata rufaa  na Sasa baada ya kupata Ambulance hii itarahisisha na wagonjwa watakuwa wanafika hospital ya mkoa kwa haraka sana" alisema Dkt. Neema.

Share To:

JOEL MADUKA

Post A Comment: