Watoa Huduma za Fedha wameshauriwa kuwapa elimu wateja wanaowahudumia ili wapate uelewa wa masharti ya mkopo ikiwemo muda wa mkopo, riba na kiwango cha kurejesha kabla ya kuchukua mkopo na kusaini mkataba ili kupunguza migogoro inayoweza kutokea baada ya huduma kutolewa.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Mikopo wa Taasisi ya Tofo Financial Services Bw. Dastan Sebastian, ambae ni mkazi katika Kata ya Mutukula wilayani Missenyi mkoani Kagera, baada ya kupata elimu ya masuala ya fedha inayoendelea kutolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
“Tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuona umuhimu wa kutoa elimu kwa Wananchi, elimu hii ikiwafikia wananchi wote itasaidia kupunguza kama sio kumaliza migogoro inayoendelea nchini”, alisema Bw. Sebastian.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mutukula, Mhe. Haji Swalehe Chakula, amewataka Wananchi wa Kata hiyo kufanya uchunguzi na kujiridhisha kama Taasisi za Fedha wanayoenda kuchukua mikopo ni rasmi ili kuepuka kuingia kwenye matatizo na mtoa huduma husika.
“Nawasihi sana Wananchi wangu msiwe wepesi kukimbilia kuchukua fedha kabla ya kusoma mkataba na kuelewa masharti ya mkopo hata kama una uhitaji wa fedha hii itasaidia kupunguza kesi zinazoendelea katika Kata yetu,”, alisema Mhe. Chakula.
Kwa pande wake mjasiriamali, mkazi wa Kata ya Mutukula wilayani Missenyi, Bi. Anna Domisiani, alisema kuwa kabla ya kupata elimu ya fedha alikua akichukua mikopo kwa mazoea bila kusoma mkataba ambayo ilikuwa ikimletea shida wakati wa kurejesho.
“Elimu niliyoipata leo itanikomboa kiuchumi lakini pia itanisaidia kuepukana na migogoro na watoa huduma, elimu hii ntaitumia kuwaelimisha wanakikundi wenzangu umuhimu wa kusoma mkataba kila karatasi na kuhakikisha wanaelewa ndipo wasaini”, alisema Bi. Domisiani.
Naye Afisa Mwandamizi Uchambuzi Masuala ya Fedha Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Gladness Mollel, alitoa elimu kwa Wananchi kuhakikisha wanasaini kila karatasi ya mkataba wanapochukua mkopo ili kuepusha kuongezwa kwa karatasi nyingine yenye masharti magumu ambayo hayatekelezeki.
Katika zoezi la kutoa elimu kwa wananchi Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Fedha imeambata na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Post A Comment: