Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ametembelea mradi wa Maji wa Kijiji cha NAFCO na kuhakikishiwa kuwa wananchi wa Monduli watapata huduma ya maji safi na salama kufikia Julai Mosi ya mwaka huu.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amepewa hakikisho hilo mara baada ya kuutembelea mradi huo na kuangalia maendeleo yake na kuwataka Wakala wa maji na usafi Vijijini RUWASA kuongeza kasi katika ukamilishaji wa mradi huo ulio muhimu kwa wananchi.
Mradi huo wa maji unazalisha Maji Lita 6000 kwa saa moja suala ambalo linatajwa kuwa litaondoa changamoto ya maji kwa wananchi zaidi ya 3500 wanaotarajiwa kunufaika na mradi huo mkubwa wa maji.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa wananchi wa pembezoni mwa mradi huo kuwa wanufaika namba moja wa mradi huo badala ya kusafirisha maji hayo kwenda maeneo mengine na kuwaacha wenyeji wa mradi huo.
Maelezo ya Mkuu wa Mkoa yamekuja mara baada ya mahojiano yake na Meneja Ruwasa Mkoa wa Arusha Injinia Joseph Makaidi ambaye anasimamia mradi huo kwa kushirikiana na wataalam wengine wa mamlaka hiyo ambapo amesema Maji hayo yatasambazwa kwenye maeneo ya zaidi ya Kilomita 12000.
Post A Comment: