Na Denis Chambi , Tanga.
WATAALAMU kutoka chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) wamebuni mashine ya 'Hydrogen Electrolized' inayozalisha gesi mbadala ya kupikia pamoja na kutumika kwenye vyombo vya usafiri ambavyo hutumia Dizeli na Petroli ambayo inakwenda kuondoa hewa ukaa inayopelekea athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazotokana na shughuli mbalimbali ikiwemo matumizi ya kuni.
Akizungumza katika uzinduzi ya maonyesho ya elimu ,ubunifu na ujuzi yaliyoshirikisha vyuo vyote vya elimu hapa nchini ambayo yanafanyika kitaifa mkoani Tanga mwanafunzi kutoka katika chuo hicho Cha MUST Lusano Luvanda amesema kuwa gesi hiyo ambayo inatokana na maji kupitia gesi ya Hydrogen pamoja na Oxygen ni salama kwa matumizi ya nyumbani tofauti na gesi nyingine zote zinazotumika kwa sasa.
"Gesi hii tulilenga kwaajili ya matumizi ya aina mbili tofauti ambayo ni nishati ya mafuta mbadala kwaajili vya vyombo vya usafiri vya moto kwahiyo badala ya kuutumia Petroli au Dizeli unaweza kutumia gesi hii inayotokana na maji bila shida yeyote na hii ni nyepesi na salama sana na rafiki kwa mazingira tofauti na mitungi mingine ya gesi "
"Kazi nyingene unaweza kutumia kwaajili ya kupikia kwa muda wowote ambapo lita moja ya maji unayotia kwenye mtambo unaweza kuutumia zaidi ya miezi miwili ikifika kiwango cha maji kitakuwa kimepungua na utaweza kuongeza na kuendelea kuutumia" amesema Luvanda.
Amesema mitambo hiyo ambayo imetengenezwa ndani ya chuo hicho kwa kupitia bidhaa nafuu imekuwa ni gharama rahisi tofauti na mitungi mingine ya gesi ambapo mwananchi wa kawaida anaweza kumudu gharama zake huku akieleza namna ambavyo itaweza kuwanufaisha watanzania wa kipato cha chini.
"Gesi ya kawaida ina bei ya juu kuliko hii tuliyozalisha ambayo haina madhara Wala uhatibifu wa aina yeyote kwa matumizi ya binadamu na mazingira tunaamini itaongeza uchumi wa Taifa na inakwenda kuondoa kabisa matumizi ya gesi ya kawaida ambayo inachafua mazingira" ameongeza.
Akifungua maonyesho hayo ya elimu ubunifu na ujuzi May 27,2024 yanayoendelea katika viwanja vya Popatlal mkoani Tanga waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Menda amesema Serikali inaendelea kuwapa kipaumbele wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi ambapo baada ya kumaliza kidato cha sita na kufanya vizuri kwenye mitihani yao watagharamikiwa kwa asilimia 100 kusoma bure vyuoni mpaka watakapomaliza.
"Tumeanzisha elimu kupitia Skolarship ya Samia Sasa Kama wewe ni mwanafunzi na unasoma masomo ya Sayansi kati ya wanafunzi bora 600-700 watakaomaliza kidato cha sita na kuamua kusoma vyuo vya ndani wanafunzi hao watalipiwa gharama zote na Serikali kwa asilimia 100 gharama zote pamoja na za kujikimu mpaka watakapomaliza masomo yao"
Akizungumzia ubunifu na ujuzi waziri Mkenda amewaasa wasanii wote hapa nchini kutumia vyema kazi zao kama nyenzo ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wakishirikiana kupinga ukatili hususani kwa watoto wa kike kuwaepusha na janga la mimba za wa utotoni.
Aidha Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea na mkakati wake wa kuwarudisha watoto wa kike shuleni ambao walikatisha masomo yao baada ya kupata ujauzito ambapo amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kupigia vita ukatili kwa watoto huku akiwataka kutokuwafumbia macho wale wote wanaowarubuni watoto wa kike na kuwapa ujauzito wakati wakiwa shuleni.
"Niwaombe sana wasanii wote hapa nchini kwa pamoja endeleeni kuhimiza vijana wapende elimu, wasome kwa jitihada na wanamaliza shule tunalo tatizo la watoto kutokumaliza shule ambalo tunalifanyia utafiti, tunalo tatizo la mabinti kupata ujauzito wakiwa shuleni na hatimaye wanaacha kusoma tunaendelea na mkakati wa kuwarudisha mashuleni ili watimize ndoto zao bado Serikali jnapenda kila mtoto asome"
Post A Comment: