Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Arusha kumkamata Bw. Simon Kaaya ambaye ni Afisa Mtendaji wa kata ya Bwawani akituhumiwa kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kwenye kata hiyo.

Mhe. Paul Christian Makonda amefikia hatua hiyo leo Mei 28, 2024 wakati akiendelea na ziara yake Wilayani Arumeru ambapo wananchi wa Kata ya Bwawani walimlalamikia Afisa Mtendaji huyo, akidaiwa kuwa ndiye sababu ya migogoro ya ardhi kwa kuuza ardhi ya Kata hiyo kwa watu mbalimbali.

Mwananchi aliyejitambulisha kwa Jina la Lucas Samwel amemuambia Mkuu wa Mkoa kuwa Mtendaji huyo amemsababishia hasara kubwa ya kifedha kutokana na kukopa fedha zaidi ya Milioni sita kwaajili ya kununua shamba alilouziwa na Mtendaji huyo na wakati Mtendaji huyo aliposikia Ujio wa Mkuu wa Mkoa alimuita Bw. Lucas na kutaka kumrejeshea Milioni tatu kati ya milioni sita ikiwa ni miaka miwili baadae.

Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, imedaiwa kuwa Afisa Mtendaji huyo amekuwa akiwatafuta watu na kuwafanya kuwa wamiliki wa ardhi ya kata na baadae Mtu huyo kuanza kuuza ardhi hiyo ikiwa ni kinyume na sheria na taratibu za ardhi.

Mapema leo asubuhi wakati wa mawasilisho ya ripoti ya wilaya ya Arumeru, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa Wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi miongoni mwa Wilaya zote sita za Mkoa wa Arusha na hivyo kumuomba Mkuu wa Mkoa kutoa usaidizi katika kutokomeza migogoro hiyo ya ardhi.







Share To:

Post A Comment: