Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewaagiza Wakala wa Ufundi na Umeme, TEMESA kufanya marekebisho ya kivuko cha MV Kitunda kinachotoa huduma ya usafiri Kwa wananchi wa maeneo ya Kitunda na Lindi Mjini.


Na Fredy Mgunda, Lindi.


Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewaagiza Wakala wa Ufundi na Umeme, TEMESA kufanya marekebisho ya kivuko cha MV Kitunda kinachotoa huduma ya usafiri Kwa wananchi wa maeneo ya Kitunda na Lindi Mjini.

Mhe. Telack ametoa maagizo hayo leo jumatano tarehe 22 Mei 2024 katika eneo la Kivuko kufuatia changamoto za kivuko hicho kushindwa kutoa huduma bora ya usafiri kutokana na kuharibika mara kwa mara.

Akizungumza na Viongozi na wasafiri, Mhe. Telack amesema kuwa kivuko hicho kimefanyiwa ukarabati hivi karibuni lakini bado ni kibovu na kimekuwa kikihatarisha usalama wa wasafiri jambo ambalo uongozi hauwezi kufumbia macho. 

Kutokana na changamoto hiyo, Mhe. Telack amesitisha huduma ya usafiri wa kivuko hicho huku akitoa muda wa wiki mbili kwa TEMESA kufanya marekebisho ya kivuko hicho ikiwemo kwenye mfumo wa injini, mfumo wa hydraulic na mfumo wa kupoza.

Pamoja na kusimamisha huduma ya kivuko hicho, amewataka TEMESA kutafuta haraka usafiri mbadala utakaotumika kuvusha wananchi upande wa Kitunda na Lindi Mjini wakati ukarabati wa MV Kitunda ukiendelea.

Kwa upande wake, Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Ndg. Abdurahaman Amir amesema kuwa utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa unaanza mara moja na tayari tathmini ya marekebisho ya kivuko imekwishaanza huku taratibu za kupata kivuko mbadala ndani ya muda mfupi ukiwa unaendelea.

Ndg. Amir ameongeza kuwa TEMESA itahakikisha marekebisho yote yanakamilika kabla ya wiki mbili kuanzia leo tarehe 22 Mei 2024 ili huduma ya usafiri kwa wananchi irejee katika ubora unatakiwa

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: