Na Mapuli Kitina Misalaba
Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Familia Duniani, Mei 15,2024, kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga imewakumbusa wazazi, walezi na jamii wajibu wa kuendelea kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Wito huo umetolewa na katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Daniel Kapaya wakati wa kikao cha pamoja na viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA Wilaya ya Shinyanga leo Mei 7,2024.
Pamoja na mambo mengine Bwana Kapaya ameendelea kuikumbusha jamii umuhimu wa kushirikiana katika hatua zote za kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aidha amesisitiza pia umuhimu wa kuwekeza kwenye malezi na makuzi ya watoto huku akiiomba jamii kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
“Katika kipindi muhimu cha kuwekeza kwenye Malezi na Makuzi ya Watoto ni umri wa mtoto akiwa tumboni mwaka (0) hadi miaka 8; umri ambao ukuaji wa ubongo wa binadamu hukua kwa takribani asilimia 90; huu ni ukuaji unaomwezesha mtoto kuwa na uwezo mkubwa wa akili ya kufikiri (darasani), kupambanua mambo, kujieleza na kutafakari mambo wakati wa utoto hadi anapokuwa mtu mzima”.
“Hakikisha afya ya mama na mtoto ipo imara, kabla na baada ya mtoto kuzaliwa ikiwa ni pamoja na kupata chanjo zote, lishe ya kutosha ya mama na mtoto, mtoto ajumuishwe mapema ili kupata ujifunzaji na uchangamshi wa awali (shule za awali) na mtoto alindwe asifanyiwe ukatili wa aina yoyote ikiwa pamoja na vipigo, maneno ya maudhi na vitendo vingine kama ubakaji na ulawiti”.
“Katika umri wa mtoto chini ya miaka 18, Mzazi au Mlezi anawajibika kuendelea kuimarisha malezi na matunzo ya motto, unawakumbusha wazazi na walezi kumpatia mtoto mahitaji yake ya msingi, kuimarisha ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili na pia kujenga tabia ya kuwasiliana au kuzungumza na mtoto mara kwa mara ili kujenga muunganiko (bond) tangu utotoni; hivyo hatua hii itawezesha mtoto kuwa na upendo kuanzia wakati wa utotoni na siku za mbeleni anapokuwa mtu mzima (ikumbukwe, wazazi wengi wanalalamika watoto hawawajali na wamekosa upendo, na hayo ndiyo madhara ya kutokuwa karibu na mtoto tangu umri wa awali)”.
“Toa taarifa ya vitendo vya ukatili wa mtoto ndani ya siku 3 kwenye vituo vya polisi ili kupatiwa msaada. Pia unaweza kupiga simu ya bure namba 116 kwa msaada na huduma zaidi”.
Katika kikao hicho baadhi ya viongozi wa SHIVYAWATA wameipongeza kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga ambapo wamesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa kampeni hiyo katika kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na serikali.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti idara ya Itifaki, uanachama na uenezi Bwana Solomon Najulwa amesema SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga itaendelea kutetea haki za watu wote bila ubaguzi.
Tarehe 15 Mei ya kila Mwaka, Tanzania huungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia ambapo maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na Kaulimbiu inayosema “Tukubali Tofauti zetu kwenye Familia; Kuimarisha Malezi ya Watoto”.
Mwenyekiti idara ya Itifaki, uanachama na uenezi Bwana Solomon Najulwa akizungumza
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ualbino (TAS) mkoa wa Shinyanga Yunice Manumbu akiwapongeza viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga.
Post A Comment: