13ad9a07-2cf4-4566-bea2-7ee2465b87a8


Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameitaka jamii na wadau mbalimbali kuweka mazingira rafiki kwenye swala la hedhi salama ili mwanamke aweze kutimiza ndoto zake bila kikwazo chochote.


Waziri Ummy ametoa wito huo leo Mei 22,2024 Jijini Dodoma wakati akitoa  Tamko kwa Umma kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Hedhi Salama na uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya  Hedhi Salama Mei 22 - 28, 2024.


"Bila Hedhi salama hakuna ustawi, kwanini tuone kinyaaa kuzungumza masuala ya  hedhi salama? Suala la hedhi salama hatuwezi kulikwepa ni sehemu ya kuendeleza kizazi katika jamii na taifa kwa ujumla,"amesisitiza Waziri Ummy.


Amesema inaposemwa hedhi salama maana yake mhusika  anapata elimu bila kikwazo, huduma katika mazingira ya vyoo, uwepo wa  usiri, uwepo maji, vifaa salama na utupaji salama wa vifaa vilivyo tumika.


Waziri Ummy amesema kila mwezi wanawake bilioni 1.9 wanakuwa katika kipindi cha hedhi kati ya watu bilioni  7 ambayo ni  asilimia 26 wengi wakiwa ni wenye miaka 15-49.


Aidha Tanzania kwa mujibu wa takwimu za watu na makazi zilizotolewa mwaka 2022 na NBS Wanawake 14.9 wanachangamoto hiyo kati ya miaka 15-49.


"Idadi hii ni kubwa hatuwezi kudharau mahitaji yao, hatuwezi kukaa kimya huu ni wajibu wetu kupata hedhi salama kuanzia ngazi ya kaya, Taasisi mpaka jamii,"ameeleza  Waziri Ummy.


Hata hivyo ameweka wazi kuwa  hedhi isiyosalama inaathari kubwa kwa jamii ikiwemo kupata magonjwa kama UTI.


Vile vile ameongeza kuwa Taasisi ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ilifanya utafiti ambapo asilimia 17 ya wasichana walishindwa kuhudhuria masomo kutokana na maumivu ya tumbo, kuogopa fedheha endapo wangechafuka na kukosa vifaa salama.


"Ni matumaini yangu leo tunapozindua maadhimisho ya Hedhi salama itakuwa ni chachu kuwekeza katika miundombinu na vifaa ili kuwafanya kuhudhuria mashuleni,"amesema Waziri Ummy.


Amesema kuna mitazamo katika jamii lakini mengine imekuwa na adhari hasi ambazo zinamnyima mwanamke katika kuchangia maendeleo.


Amesema masuala hayo hayawezi  kumalizwa katika siku Moja serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuwekeza na kutekeleza afua mahususi ili kuhamasisha kuondoa tabia zinazoanda unyanyapaa kuanzia katika ngazi ya kaya.


Pia Wizara inakamilisha muongozo wa Hedhi salama ambao utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali katika jamii.


Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuweka mikakati ili kuweka utaratibu mzuri kwa msichana upatikanaji wa mahitaji muhimu bila kikwazo.


Amesema kila ifikapo Mei 28 kila mwaka Tanzania inaungana na Nchi zingine  Dunia kuadhimisha  siku ya Hedhi Duniani ambapo kwa Tanzania wataadhimisha wiki nzima kuanzia Mei 22 hadi 28 mwaka huu Jijini Arusha.


Waziri Ummy amesema wamekuwa wakiadhimisha tangu mwaka 2015 lengo likiwa  ni  kuhabarisha na kuvunja ukimya kuhusu masuala ya hedhi  salama katika kuendeleza kizazi.

0de0b5d7-200e-4c82-960b-fb7646e098ae

1d71f672-3d09-4e0d-9911-cacb380e477b

4cbc2f5d-f0df-4d5c-bb07-5d1eac53914a

c26aac84-6627-404b-a41c-bfdcdffe446b

c28b0e10-2d4d-4ca8-bb53-aa368f83b95f
Share To:

Post A Comment: