Imeelezwa kwamba kukamilika kwa ujenzi wa Barabara ya Km. 30.3 kutoka Sawala -Mkonge- Iyegeya uliogharimu shilingi bilioni 12.17 kupitia mradi wa Agri- Connect unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) umeongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya mbogamboga, chai na kahawa kwa wakulima wa wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Meneja wa TARURA wilaya ya Mufindi Mhandisi Richard Sanga alipozungumza na waandishi wa habari katika mashamba ya chai wilayani hapa.
Mhandisi Sanga amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kumeongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya wakulima wilayani hapo ambapo awali mazao yao yalikuwa yanaharibika njiani kabla ya kufika viwandani na hivyo wananchi hao na vyama vya ushirika kupata hasara kubwa.
“Lengo kubwa la mradi huu ilikuwa kuwawezesha wakulima kutoa mazao yao mashambani na kufikisha viwandani yakiwa na hali nzuri kwani kabla ya mradi huu kutekelezwa mazao ya wananchi hasa chai yalikuwa yanaharibika njiani kabla ya kufika viwandani hususan kipindi cha mvua na hivyo kudhorotesha uchumi wa mwanachi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”
“Tunashukuru kwa kupata mradi huu kwani kukamilika kwa barabara Km. 30.3 kumewezesha wananchi kukua kiuchumi na kuongeza tija katika uzalishaji pamoja na kurahisisha shughuli za usafiri kwa wakazi wa maeneo mengine yanayozunguka mradi huu zikiwemo kata za Mtwango, Luhunga, Ihanu na Mdabulo kwani awali usafiri ilikuwa ni changamoto”. Aliongeza Mhandisi Sanga
Aidha, Mhandisi Sanga aliongeza kusema kwamba jumla ya barabara hiyo ni km 40.7 hivyo Km. 10.4 zilizobaki sasa hivi wanaendelea na matengenezo kwa kiwango cha lami kwa kutumia teknlojia mbadala ya ‘Ecoroads’.
Amesema TARURA wanaendelea kuhakikisha barabara zote wanazozisimamia zinapitika katika majira yote na wananchi wake wanasafiri na kusafirisha mazao yao ili kuwainua kiuchumi wananchi wake.
Naye Bw. Santino Mdeta mkulima wa chai kutoka kijiji cha Mkonge amesema kata ya Luhunga vipo vijiji vingi vinavyolima chai hivyo wanaishukuru Serikali kupitia mradi wa Agri-connect kwa kuwasaidia Barabara ambayo ilikuwa changamoto kubwa sana kwa wakulima wa zao hilo.
Amesema kabla barabara haijatengenezwa ilikuwa changamoto kubwa sana kwani chai zilizokuwa zikichumwa Kwenda kiwandani zilikuwa zikifika kwa shida kwa kuwa zao hilo linahitaji kufikishwa kiwandani ndani ya masaa nane mara baada ya kuchumwa.
Amesema walikuwa wakipata hasara kubwa kwani chai zilikuwa zikifika kwa shida viwandani na katika kipindi cha mvua ilikuwa ni hasara kwa mkulima kwani zao hilo mara nyinyi huchumwa kipindi cha masika ambapo mvua zinakuwa ni nyingi na kusababisha kutokufika kwa wakati.
Post A Comment: